Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi pamoja na Watendaji wa Mamlaka ya uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar { ZIA } kuwa wabunifu katika kuandaa utaratibu mzuri unaokwenda na wakati ambao utaondoa usumbufu kwa wasafiri wanaotumia uwanja huo.

Alisema watendaji hao pia wanapaswa kubadilika na kwenda na wakati kulingana na huduma wanazotoa kwa wasafiri hasa wakizingatia kwamba uwanja huo hivi sasa unaendelea kuimarishwa katika hadhi na kiwango cha Kinachokubalika kimataifa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya ghafla kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kufuatia malalamiko mbali mbali aliyokuwa akiyasikia kutoka kwa baadhi ya abiria kutokana na huduma zinazotolewa uwanjani hapo .

Matatizo yanayolalamikiwa zaidi na abiria hao ni pamoja na umbali wa masafa kati ya eneo la maegesho ya gari na lilipo jengo la wafafiri ambapo hujitokeza usumbufu kwa wale wasafiri wenye mizigo mikubwa pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa hasa wakati wa mvua.

Balozi Seif alisema utaratibu uliopo hivi sasa ni vyema ukaimarishwa zaidi ili kupunguza bughdha pamoja na kuwapa faraja abiria ambao wengi kati yao huwa tayari wameshachoka kutokana na uchovu wa safari zao za Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwatahadharisha watendaji hao kuwa makini na kauli zao wakati wanapotoa huduma kwa wasafiri wao ili kuwaondolea shaka na dhana wakati wanapoamua kutembelea hapa Zanzibar.

“ Zipo taarifa kwamba baadhi ya watendaji wamekuwa na kauli za makaripio. Sasa umefika wakati kwao kuwapunguzia bughdha wateja wao ili isionekane msafiri anayetembelea Zanzibar akaanza kuweka simanzi “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar uliutaka uongozi huo wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kukaa pamoja na Idara ya Uhamiaji pamoja na taasisi nyengine zinazokusanya mapato kiwanjani hapo katika kulitafutia ufumbuzi wa haraka tatizo la urasimu unaosababisha msongamano mkubwa wa wasafiri.

Alisema msongamano huo unaweza kuepukwa kwa taasisi hizo kuweka utaratibu utakaotoa huduma kwa ubia badala ya ule uliopo hivi sasa wa msafiri kupanga foleni ya kupata huduma kwa kila Taasisi.

Balozi Seif aliuhakikishia uongozi wa Mamlaka hiyo kwamba Serikali itajitahidi kuona yale mapungufu yanayokwaza uwajibikaji wa watendaji wa taasisi hiyo ambayo husimamiwa na taasisi nyengine yatapatia ufumbuzi.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar Nd. Said Iddi Ndombogani alisema mamlaka hiyo inaendelea na juhudi za kukamilisha matengenezo ya banda la wasafiri litakalokidhi mahitaji hasa wakati wa msimu wa masika.

Nd. Said alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba malalamiko ya abiria kuteremka mbali na eneo la kupata huduma za wasafiri litakamilika baada ya kumalizika kwa matengenezo hayo.

Alisema utaratibu utawekwa kwa abiria hao kujihudumia wenyewe kwa kutumia vigari maalum ili kuondosha usumbufu kwa wale wasafiri watakaokuwa na mizigo mizito au mingi katika safari zao.

“ Kama tutaruhusu magari ya abiria na yale ya wasafiri kuingia na kusimama kwa ajili ya kuteremsha wateja wao mbele ya jengo la huduma za wasafiri ni kusema kwamba foleni ya gari hizo itaongeza usumbufu na kuwachanganya zaidi wasafiri wanaotaka kuwahi kwa mujibu wa tiketi zao “. Alisema Nd. Said Iddi Ndombogani.

Alifahamisha kwamba Mamlaka inaendelea kuzingatia vigezo vya Kimataifa katika kutoa huduma kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa anga ambao humtaka abiria anayesafiri ateremke kwenye gari masafa ya mita mia Moja na eneo analotakiwa kupata huduma kwa ajili ya safari yake.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pilim wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top