Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa watendaji wote wa taasisi za umma kujituma, kuwa makini na kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa ili kuhakikisha kwamba vipaumbele vilivyowekwa na Serikali katika sekta ya uchumi na ustawi wa jamii vinatekelezwa kwa ufanisi.

Akifunga mkutano wa 16 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliojadili bajeti ya Serikali ya Mwaka 2014/ 2015 kwenye ukumbi wa Baraza hilo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali itajitahidi kuona nyenzo hasa fedha kwa ajili yab utekelezaji wa vipaumbele hivyo zinapatiklana kwa wakati.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaimarisha ukusanyaji wa kutoka katika vianzio vyake sambamba na udhibiti wa uvujaji wa mapato katika taasisi na maeneo yote ili azma iliyokusudiwa iweze kufikiwa vyema.

Balozi Seif aliwasisitiza Wafanyabiashara pamoja na wananchi kujenga utamaduni wa kulipa kodi na ada katika huduma zote za kiuchumi na kijamii lengo likiwa ni kuiongezea mapato Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa malengo yake iliyojipangia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali imejipanga kuimarisha miundombinu ya kiuchumi pamoja na huduma za Kijamii kama vile elimu, afya bora na upatikanaji wa huduma za maji safi na salama.

Alieleza kwamba hatua hiyo itakwenda sambamba na uimarishaji wa huduma za makundi maalum hasa kwa wazee wasiojiweza, watoto na watu wenye ulemavu pamoja na kuimarisha mazingira ya biashara kwa kuondosha vikwazo visivyo vya lazima.

Akizungumzia suala la migogoro ya ardhi linaloonekana kuongezeka kutokana na kui8marika kwa shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii Balozi Seif alisema Serikali itaendelea kuchukuwa juhudi katika kuhakikisha migogoro hiyo inapungua na hatimae kuondoka kabisa.

Alisema zipo dalili zilizobaina ambazo zimeonyesha wazi kuwa baadhi ya migogoro ya ardhi iliyopo katika maeneo mengi hapa nchini inasababishwa na wanasiasa wachache wanaopenda kujipatia umaarufu pamoja na kutawaliwa na ubinafsi.

Balozi Seif alisema umuhimu wa ushirikiano kati ya masheha,madiwani, viongozi wa serikali, wanasiasa na wananchi unahitajika wakati Serikali Kuu inaendelea na ukamilishaji wa mpango wake wa matumizi bora ya ardhi utakaosaidia kupunguza migogoro iliyojitokeza.

“ Naamini kwamba kama sote tutashirikiana kwa dhati kwa nia ya kuiondoa migogoro ya ardhi iliyojichomoza tutafanikiwa kwa kiwango kikubwa “. Alisema Mkuu huyo wa shughuli za Serikali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwasihi wananchi wenye tabia ya kubeza wawekezaji waliopata fursa ya uwekezaji miradi yao nchini kuwacha kuwabughudhi kwa vile tayari wamesharidhia kushirikiana na Serikali katika kukuza uchumi.

Alisema Serikali imejitahidi kuwavutia wawekezaji kuitumia nafasi hiyo nia ikiwa ni kuongeza mapato ya serikali pamoja na kupunguza mfumko wa vijana wasio na ajira.

Kuhusu suala la amani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali imesikitishwa na kitendo cha kihalifu kilichotokea hivi karibuni cha mripuko wa bomu kwenye eneo la Darajani MjiniZanzibar ambapo mtu mmoja aliuawa na wengine saba kujeruhiwa katika mripuko huo.

Alisema tukio hilo ni la kushtusha, kusikitisha na Serikali inaendelea kulaani kwa nguvu zote kitendo hicho cha kihaini huku ikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa kuendelea kuwasaka wahalifu waliohusika na tukio hilo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Balozi Seif aliwathibitishia wananchi pamoja na wageni wote waliopanga kuitembelea Zanzibar kwa Visiwa vya Unguja na Pemba bado viko katika hali ya usalama, amani na utulivu. Hivyo ni vyema wakaendelea na harakati zao za kimaisha bila ya hofu.

Alieleza kwamba licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kuenzi umoja, amani na utulivu nchini lakini bado Viongozi na Wananchi wanapaswa kutowapa nafasi wale watu wanaochochea mifarakano ambayo inaweza kuvuruga nchi na kudumaza maendeleo ya wananchi.

“ Hatutavitendea haki vizazi vyetu kama tutaiacha nchi hii kudumbukia katika wimbi la vurugu na uvunjifu wa amani “. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Akielezea masikitiko yake kutokana na mahudhurio yasiyoridhisha ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kufikia hatua ya spika kuahirisha baadhi ya wakati Balozi Seif alisema hilo ni jambo lisilokubalika kidemokrasia, kiuchumi, kisiasa na linalidhalilisha baraza hilo.

Alisema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni macho, masikio na midomo ya wananchi wanaowawakilisha majimboni mwao. Hivyo kuendelea kwa kitendo hicho ni kuwanyima haki wananchi waliowachagua.

Malozi Seif alionya kwamba utoro huo unaopelekea kuahirishwa kwa vikao hivyo vya Baraza la Wawakilishi vinapoteza fedha nyingi za walipa kodi ambao ni wananachi.

“ Hatuoni kama ni unafiki tunapopiga kelele kuwa Serikali inapoteza fedha za wananchi wakati sisi wenyewe pia tunachangia upotevu huo ? “. Alikemea Balozi Seif.

Katika Mkutano huo wa 16 wa Baraza la Nane la Wawakilishi uliojadili Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2014/2015 jumla ya maswali ya msingi 66 na mengine 183 ya nyongeza yalioulizwa na waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kujibiwa na Mawaziri wa Sekta husika.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi siku ya Jumatano ya Tarehe 22 Oktoba mwaka huu wa 2014 mnamo saa 3.00 za asubuhi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top