Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini wamehimizwa na kukumbushwa kuendelea kumcha Mwenyezi Muungu hasa katika kipindi hichi cha kumi la mwisho la mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambacho kimepata baraka ya kuwemo kwa usiku wenye chezo wa Lailatul Qadri.

Himizo na kumbusho hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idriss Muslim Hija kwa Niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Balozi kwa Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.

Futari hiyo ya pamoja iliyoshirikisha pia baadhi ya viongozi wa Dini ya Kiislamu na watu maarufu na mashuhuri wa Mkoa huo ilifanyika katika viwanja vya jengo la Idara ya Uhamiaji iliyopo Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Dr. Idriss Muslim Hija ni vyema kwa waumini hao wakajipinda vilivyo na kuacha usingizi wao badala yake waelekeze nguvu zao katika kufanya ibada ili wasipitwe na usiku huo mtukufu wenye cheo.

“ Ni vyema usingizi katika kumi hili tukauweka pembeni ili tupate wasaa zaidi wa kuongeza nguvu katika ibada ndani ya mfungo huu mtukufu “. Alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wa Kusini Unguja.

Aliwahimiza waumini na Wananchi hao kuhakikisha kwamba yale mafunzo na maelekezo waliyoyapata ndani ya kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wanayaendeleza katika vipindi vyengine vijavyo.

Akitoa shukrani Diwani wa Wadi ya Koani Nd.Shaaban Jabu Kitwana kwa niaba ya wananchi na waumini wenzake wa Mkoa wa Kusini Unguja alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa uamuzi wake kujumuika na wananchi kwenye futari ya pamoja katika mikoa mbali mbali hapa nchini.

Nd.Shaaban alisema hatua hiyo ya Balozi Seif mbali ya kuleta mapenzi ya upendo lakini pia inaongeza ukaribu na ushirikiano kati ya wananachi pamoja na viongozi wanaowaongoza.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top