Uongozi wa Mradi wa uwekezaji wa sekta ya utalii unaosimamia uendeshaji wa hoteli za Kitalii zilizomo ndani ya visiwa vidogo vidogo vya Bawe na Changuu { Bawe leisure hotel na Changuu Leisure hotel } umehimizwa kujitahidi kuongeza vivutio vya utalii vinavyopendwa na wageni ili kuzidi kuimarisha mapato ya Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa himizo hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua shughuli za uwekezaji na hifadhi ya mazingira katika visiwa hivyo vilivyopo pembezoni mwa bahari magharibi ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif akiambatana na Uongozi wa juu wa Wizara ya Habari, Taasisi za mazingira, mamlaka ya uwekezaji vitega uchumi na baadhi ya maafisa wa serikali aliueleza Uongozi wa mradi huo ulio chini ya Kampuni ya Mafuta ya Gapco kwamba Serikali imekusudia kuimarisha sekta ya Utalii ili ifaidishe vipato kwa pande zote husika.

Aliupongeza Uongozi wa Bawe na Changu Leisure Hoteli kwa umakini wake katika uendelezaji wa sekta ya utalii unaozingatia hifadhi ya maumbile ya mazingira yaliyomo ndani ya visiwa hivyo viwili.

“ Nimefarajika na jitihada zenu za kuuendeleza mradi huu mkubwa wa utalii. Eneo la Bawe na Changuu maumbile yake yanafanana kama Mji mpya wa Malawi wakati unaanzishwa ukizingatia uhifadhi ya maumbile yake “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa Serikali na washirika wake wote kuendelea kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye sekta hiyo ambayo mafanikio yake pia yanakwenda sambamba na utoaji wa nafasi za ajira hasa kwa vijana.

Mapema Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Leisure Hoteli Bwana Freddy Tenga alisema mradi huo wa hoteli Bawe na Changuu ulianza mnamo Mwezi Disemba mwaka 2002 kwa hatua ya matengenezo ya nyumba , huduma muhimu pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Bwana Tenga alisema Uongozi wa Mradi huo umeweka mikakati ya kuimarisha huduma zake kwa kuongeza ubora na hadhi ya vyumba na chakula ili kutoa fursa ya mapumziko na utulivu mzuri kwa watalii na wageni wanaoamua kuvitembelea visiwa hivyo.

Hata hivyo Mkurugenzi wa uendeshaji wa Mradi huo wa Leisure Hotel alisema zipo baadhi ya changamoto zinazopunguza uzuri na haiba ya visiwa hivyo zinazotokana na uharibifu wa matumbawe.

Alisema uharibifu huo hufanywa na baadhi ya wavuvi wanaoamua kupiga dago sehemu hizo na huamua kutumia mitego haramu na nyavu za kukokota wakati wanapovua hali ambayo pia huhatarisha usalama wa watalii na wageni.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema Serikali bado imelenga kutoa kipaumbele kwa wawekezaji wazalendo katika kuimarisha sekta ya uwekezaji vitega uchumi nchini.

“ Tumeshuhudia Mradi wa Leisure Hoteli unavyoendeshwa na wazalendo ulivyokuwa mahiri katika uwekezaji ambao umelenga kuhifadhi makobe sambamba na utunzaji wa mazingira “. Alisema Waziri Mbarouk.

Alifahamisha kwamba Wizara ya Habari, Utamaduni Utalii na Michezo inakusudia kuandaa mpango maalum utakaopelekwa Serikalini kwa ajili ya kuvipatia baraka za hifadhi ya Taifa visiwa mbali mbali vya Zanzibar ikiwemo Bawe, Changuu na Tumbatu.

Waziri Mbarouk alieleza kwamba mpango huo ili ufanikiwe vyema taratibu zitaandaliwa katika kuwakutanisha wawakilishi wa taasisi zote zinazohusika na sekta za utalii, mazingira, historia, ardhi, Utalii, Mamlaka ya uwekezaji vitega uchumi pamoja na utamaduni kwa ajili ya kuweka mkakati wa kufanikisha mpango huo.

Mradi huo wa uwekezaji wa sekta ya utalii unaosimamia uendeshaji wa hoteli za Kitalii za Bawe na Changuu { Bawe leisure hotel na Changuu Leisure hotel } tayari umeshagharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milionio 23,000,000 katika kuzifanyia matengenezo nyumba za wageni pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Matengenezo hayo yamekwenda sambamba na utunzaji wa makobe wakifikia 132 hivi sasa wakiwa katika kisiwa cha Changuu idadi inayozidi kuongezeka kutokana na ulinzi wa kutosha uliopo katika visiwa hivyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top