Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini kujenga dhamira ya kudumisha udugu na Umoja miongoni mwao kwa lengo la kustawisha Taifa lenye nguvu kiimani.

Alisema Taifa lenye mifarakano miongoni mwa waumini na wananchi wake hata nafasi ya kufanya ibada kwa utulivu hukosekana kwa vile kila mtu hutumia muda mwingi kutapia roho yake.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohd Gharib Bilal wakati akiiahirisha rasmi jitimai ya 20 ya Kimataifa iliyokuwa ikifanyika makao makuu ya Jumuiya ya Fiy Sabilillah Markaz iliyopo Fuoni Migombani Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya waumini kuona muda wote wamekuwa wakibeba bendera ya kuhubiri utengano wakati kitabu cha Quran na hadithi zake zimekuwa zikisisitiza suala la umoja miongoni mwa waumini wenyewe.

“ Kama Mtu ni muumini wa kweli visingizio hivi wanavyopenda kuvitumia ndugu zetu hawa vinaweza vikawatoa machozi “. Alisema Balozi Seif.

Alieleza kwamba ni wajibu kwa kila muumini wa dini ya Kiislamu kulichukulia kwa uzito unaostahiki jambo hili la Umoja na Udugu wa Kiislamu, vyenginevyo watakuwa waumini wenye kupata hasara kubwa siku ya hukumu.

Akizungumzia suala la elimu ya dini na ile ya Dunia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa madrasa zilizopo nchini kufikiria kutumia mtandao wa kompyuta katika kufundishia dini ya Kiislamu.

Alisema wakati huu walimu hao wanaweza kufundishia dini ya kiislamu kwa urahisi zaidi kupiti mtandao huo kuliko wakati mwengine wowote uliopita hapo nyuma.

Alifahamisha kwamba kwa kutumia mitandao hiyo watoto wa madrasa hizo wanaweza kusikiliza vizuri video za Quran na tafsiri za aya mbali mbali watakazoandaliwa kwa undani zaidi.

Hata hivyo Balozi Seif alitahadharisha kwamba yapo baadhi ya mambo yenye kuleta hasara yanayopatikana katika mitandao hiyo ambayo yanakwenda kinyume na mafundisho na maadili ya dini hiyo.

Alitoa ushauri kwa walimu watakaohusika na elimu ya mitandao kuielewa vyema elimu hiyo ili wajue mbinu za kuwaasa vijana mambo yasiyofaa kutumiwa na wanafunzi hao kwenye mitandao hiyo.

“ Hii ina maana kwamba maovu yaliyomo kwenye mitandao ya kompyuta yatafundishwa vizuri na walimu wetu wenye uelewa mzuri wa elimu hiyo ya kompyuta “. Alifafanua Balozi Seif.

Aliupongeza Uongozi mzima wa Kamati ya maandalizi ya Ijitimai hiyo kwa maandalizi mazuri yalisaidia kufanikisha vyema ijitimai hiyo ya kimataifa iliyoshirikisha waumini wa Kiislamu kutoka mataifa ya mwambao wa afrika mashariki.

Alieleza kuwa faida kubwa itapatikana kwa umma wa kiislamu iwapo washiriki wa ijitimai hiyo watayaeneza vyema mafundisho waliyoyapata kwenye mkusanyiko huo wa ijitimai ambao ni sawa na chuo kikuu kutokana na mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na masheikh mbali mbali.

Akitoa Taarifa katibu wa Jumuiya ya Fiy Sabilillah Markaz Zanzibar Sheikh Mwalimu Hafidh Jabu alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuasisiwa kwa jumuiya hiyo miaka 20 iliyopita.

Sheikh Jabu alisema Markaz ya ijitimai Fuoni Kibondeni inatarajia kuanzisha darasa la kumi na Tatu na kumi na nne hapo mwakani kutokana na wanafunzi wa skuli yake ya Raudha kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao.

Hata hivyo katibu wa Jumuiya hiyo ya Fiy Sabilillah Markaz alisema kwamba bakora ndogo ndogo ndani ya skuli hiyo bado zinaendelea kutumika ili kulinda na kudumisha mila, silka na utamaduni wa kiislamu skulini hapo.

Aliwaomba waumini mbali mbali wa dini ya kiislamu kuendelea kuchangia huduma za ujenzi wa majengo ya akina mama pamoja na lile la wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la kumi na tatu hapo mwakani.

Mapema Amiri Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Ali Khamis Ali alisema lengo la kuanzishwa kwa skuli ya Raudha ndani ya jumuiya hiyo ni kuzalisha Viongozi bora na madhubuti watakaousimamia uislamu hapo baadaye.

Alisema skuli hiyo imekuwa tishio kubwa hivi sasa dhidi ya skuli nyengine mbali mbali hapa Zanzibar kutokana na ubora wa wanafunzi wake.

Akigusia suala la amani ambalo limekuwa likisisitizwa mara kwa mara ndani ya uislamu Amir Ali Khamis alitanabahisha kwamba hakuna mbadala katika suala hilo ambalo ni adimu kupatikana katika baadhi ya nchi duniani hasa zile nchi jirani za afrika mashariki.

Alieleza kwamba upendo, furaha na baraka ndani ya jamii hutoweka wakati inapokosekana amani katika maeneo mbali mbali ya umma.

Maelfu ya waumini wa dini ya kiislamu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara, Nchi jirani za Kenya, Uganda, Malawi, Msumbiji na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo { DRC } walishiriki katika ijitimai hiyo ya 20 ya kimataifa hapa Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


0 comments:

 
Top