Utamaduni wa Watu wa Zanzibar unaofanana na wenzao wa Pwani ya ukanda wa Afrika Mashariki bado utaendelea kuwa kielelezo cha uhusiano wa mafungamano yaliyoko baina yake na Mataifa mbali mbali Ulimwenguni .

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizindua rasmi sherehe za Tamasha la 17 la Kimataifa la Filam Zanzibar { ZIFF } hapo katika ukumbi wa Ngome Kongwe uliopo mtaa wa Forodhani Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema silka, mila na Tamaduni zinazowaunganisha wakazi wa ukanda wa Mwambao wa Afrika Mashariki umetoa fursa kubwa kwa Watu hao wapatao Milioni 150,000,000 kuwasiliana vyema kupitia lugha fasaha ya Kiswahili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Tamasha la Kimataifa la Filam Zanzibar { ZIFF } pamoja na washirika wake kwa juhudi zao za kuendelea kuitangaza Zanzibar, Tanzania na Afrika Mashariki kwa Ujumla katika Nyanja za Kiutalii Duniani.

Alisema Ziff kwa msaada mkubwa wa wafadhili wake Taasisi zilizojitolea kukuza Vipaji vya wasanii Tanzania za ZUKU na Wananchi Group imesaidia sana kuifanya Tanzania kuwa maarufu Duniani kupitia Tasnia ya sanaa hasa ile Michezo ya kuigiza.

Alifahamisha kwamba Serikali imefarajika kuona soko la Filam ndani ya Tanzania linaendelea kuwa kubwa na kutoa fursa nzuri za ajira hasa kwa kundi kubwa la Vijana.

“ Taasisi ya ZUKU imefanya kazi kubwa sana katika kusaidia vijana katika tasnia ya filam na cha kufurahisha zaidi asilimia 8% ya rasilmali zinazotumika katika Tamasha hilo ni zile za asili “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi wa Tamasha na Kimataifa la Filam Zanzibar kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari wakati wote kupokea mawazo na maoni yake katika misingi imara ya kuyajengea uwezo wa ajira makundi ya Vijana kupitia sanaa ya Filam.

“ Serikali imefarajika na kazi kubwa zinazofanywa na Tamasha la Kimataifa la Filam Zanzibar { ZIFF } katika kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla Kiutamaduni Duniani “. Alieleza Balozi Seif.

Mapema Mwakilishi wa Taasisi ya Wananchi Group ambayo ndio mfadhili mkubwa wa Tamasha la Kimataifa la Filam Zanzibar Bwana Mohd Jeneby alisema Taasisi hiyo imeamua kujitolea kunyanyua vipaji vya wasanii Nchini Tanzania.

Bwana Mohd alisema Taasisi hiyo katika mpango wake wa miaka Kumi imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni Moja ili kutoa mafunzo, warsha na mafunzo mengine kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kimaarifa wasanii hao.

Alisema mpango huo unakwenda sambamba na kujengewa uwezo kwa wasanii wa Kenya, Uganda na baadaye mwaka huu itafuatiwa na Mataifa ya Malawi na Ethiopia.

“ Tumelenga kuwapatia warsha na mafunzo wasanii wetu wa Afrika mashariki kupitia Lugha yetu maarufu na fasaha ya Kiswahili ambayo husaidia kutoa ajira kubwa kupitia sekta ya Utalii na Burdani “. Alisema Bwana Mohd Jeneby.

Ufunguzi wa Sherehe za Tamasha la 17 la Kimataifa la Filam Zanzibar { ZIFF } zitakazoendelea hadi Tarehe 22 June mwaka huu wa 2014 ulipambwa kwa burudani safi iliyokuwa ikitumbuizwa na Kikundi cha Utamaduni cha Tanuri Group kutoka Nchini Misri.

Nchi ya Misri ni miongoni mwa washirika wakuu wa Tamasha la Kimataifa la Zanzibar tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1997.

Washiri walioshuhudia ufunguzi huo kutoka nchi mbali mbali Duniani pia walishuhudia filamu maarufu iitwayo Long Walk to Freedom inayoelezea maisha ya ukombozi wa Afrika ya Kusini chini ya jemedari wake Marehemu Mzee Nelson Mandela.

Filam hiyo imetengenezwa na msanii maarufu wa Afrika Kusini na Duniani Bibi Moe Ferry Feto.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top