Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda unakusudiakutaka kujenga kiwanda chengine cha Sukari Ukanda wa Maeneo huru ya uwekezaji Vitega Uchumi yaliyopo Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba katika azma yake wa kuwekeza miradi ya Kiuchumi hapa Zanzibar.

Uamuzi wa kuanzisha mradi huo mpya umekuja kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatilana mara baada ya kuanza rasmi kwa uzalishaji wa Sukari katika Kiwanda cha Mahonda kiliopo Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Meneja Mkuu wa Mradi huo wa Kiwanda cha Sukari Pemba { Pemba Talon Sugar Factory ltd – PTSFL } Bwana Satish Purandare alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Satish alisema Uongozi wa Mradi huo unakusudia kuanza kutoa elimu kwa Wananchi wa Maneo ya Kiuyu, Micheweni pamoja na Wete wale watakaoamuwa kujishughulisha na ukulima wa Miwa ili baadaye wapate fursa ya kukiuzia miwa yao Kiwanda hicho ili kiendeshe uzalishaji wa Sukari.

Alisema kazi ya uzalishaji wa miwa itakuwa ikiendeshwa na wananchi watakaokizunguuka kiwanda hicho ili kutoa fursa ya ajira itakayowawezesha kujipatia kipato na kupunguza umaskini.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa PTSFL alimueleza Makamu wa mPili wa Rais wa Zanzibar kwamba harakati za ujenzi zinatarajiwa kuanza rasmi mapema mwaka ujao baada ya kukamilika kwa taratibu zote za uwekezaji.

“ Tumepanga kuanza shughuli za ujenzi wa Kiwancha hicho cha Sukari katika eneo huru la uwekezaji vitege uchumi liliopo Micheweni kati kati ya mwaka ujao ambapo matarajio yetu ni kuanza uzalishaji wa sukari mwezi Oktoba mwaka 2015 “. Alifafanua Bwana Satish.

Alifahamisha kwamba Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha sukari Tani 1200 kwa kiwango cha ekari 300 watakazolima wakulima na wananchi hao ikiwa ni hatua ya awali ya kuanza kwa mradi huo.

Bwana Satish alieleza kwamba mrdi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni { U$ 15,000,000 } kwa ujenzi wa Kiwanda na Doma Milioni Tano zitahusika katika uzalishaji wa mashamba utaosimamiwa na Wakulima binafsi.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda kwa hatua iliyofikia ya kuanza kwa uzalishaji wa Sukari.

Balozi Seif alisema hatua hiyo ambayo inafaa kupongezwa ni matunda mazuri yanayoanza kuchomoza ambayo mbali ya kuongeza mapato ya Taifa lakini pia yamesaidia kutoa ajira kwa baadhi ya wananchi hapa Nchini.

“ Mradi wenu mnaotaka kuutekeleza Micheweni Pemba ni matunda mazuri ya mradi mliouanzisha awali wa uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha Mahonda ambao tayari umeanza kutoa faida “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba ongezeko la ujenzi wa viwanda vya sukari kwa kiasi Fulani litasaidia kupunguza mfumko wa bei ya bidhaa hiyo kiholela hapa Nchini.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumzo na Rais wa chuo Kikuu cha Franklin Columbus kilichopo Jimbo la Ohio Nchini Marekani Dr. Godfrey Mendes.

Katika mazungunzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar Dr. Godfrey Mendes alimuelezea Balozi Seif azma ya Chuo Kikuu hicho ya kutaka kujenga Kampas yake hapa Zanzibar.

Dr. Mendes alisema Franklin University Columbus, Ohio USA imekuwa ikitoa huduma za elimu ya juu ya vyuo vikuu katika masomo ya Sayansi, Komputer, Ustawi wa Jamii katika Mataifa 12 Duniani.

Alifahamisha kwamba Uongozi wa Chuo hicho umeridhika na hali ya mazingira na utulivu wa Zanzibar na kufikia azma ya kutaka kuanzisha kampas ya chuo hicho hapa Zanzibar itakayoshirikisha wanafunzi kutoka nchi mbali mbali Duniani.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea kukaribisha wawekezaji wa sekta mbali mbali za kiuchumi, ustawi wa Jamii na zaidi masuala ya elimu.

Katika kujiimarisha kuzalisha wataalamu wazalendo NCHINI Balozi Seif alisema Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kinaendelea na mikakati ya kufundisha mafunzo ya Udaktari sambamba na fani ya kilimo ili kuondosha upungufu wa wataalamu katika fani hizo mbili muhimu kwa ustawi wa Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa Chuo hicho Kikuu cha Franklin Columbus Ohio cha Nchini Marekani kuwasiliana na Uongozi wa chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } katika kutafuta mbinu za kufanikisha mipango hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top