Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alisema Jukumu la Serikali liliopo wakatio huu ni kujiandaa na ongezeko la idadi ya watu linalokadiriwa kufikia Milioni Mia 125,000,000 ifikapo mwaka 2050.

Dr. Kiwete alieleza wakati akizindua chapicho la tatu la Taarifa za msingi za Kidemografia, Kijamii na kiuchumi linalotiokana na sense ya watu na makazi ya mwaka 2012 pamoja na matumizi ya Tovuti katika kupata taarifa mbali mbali za sensa ya watu na makazi.

Hafla hiyo fupi ikiwa ni mfululizo wa machapisho mbali mbali yanayotolewa na Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa na watu na makazi ilifanyika katika Ukumbi wa Seluu wa Jumba la Kimataifa la Mikutano la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere liliopo Mtaa wa Shaban Robert Jijini Dar es salaam.

Alisema Takwimu zinazotokana na zoezi la sense ya watu inayokuwa ikifanyika kila baa ya miaka kumi nchini husaidia kuliamsha taifa jinsi ya kujipanga vyema katika utekelezaji wa majukumu yake sambamba na kuwa makini katika kukabiliana na changamoto zinazolikabili taifa.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alitahadharisha kwamba ongezeko la idadi ya watu nchini linatisha na kuketa hofu kwa vile haliendi sambamba na ukuaji wa uchumi wake kasi ambayo inaweza kuleta balaa hapo baadaye.

“ Tuangalie takwimu zetu zinavyotuonyesha kuhusu ongezeko la haraka la idadi ya watu, ukuaji wa miji yetu pamoja na kuzidiwa cha huduma za kijamii kutokana na maongezeko hayo jambo ambalo ni hatari na linahitaji kazi ya ziada katika kukabiliana nalo “. Alieleza Dr. Kikwete.

Akizungumzia juhudi za seikali katika kujenga mazingira mazuri ya kila Mtanzania kuishi maisha ya wastani Rais Kikwete alisema Serikali iko katika mipango ya miaka mitano itakayoliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kati na kati.

Alisema hivi sasa juhudi zimelenga kuendelea na mpango wa Pili wakati ambapo ule wa tatu unatarajiwa kukamilikwa mwaka 2025 kupitia mpango wake wa maendeleo wa 2025.

“ Taifa sasa linaingia katika katika matumizi makubwa ya kukusanya Taarifa za Takwimu baada ya kuelewa faida na umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa na Jamii yote “. Alisisitiza Dr. Kikwete.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alifahamisha kwamba maendeleo yoyote yale lazima yazingatie usawa wa Kijinsia jambo ambalo wanawake wanastahiki kupata haki zote wanazostahiki baada ya kuzikosa kwa kipindi kirefu kutoka na mfumo dume iliokuwa ukitumiwa.

Akimkaribisha Mgeni rasmi Rais Kikwete Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa na Watu na Makazi ya Mwaka 2012 Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda alisema machapisho yote yaliyotolewa yana lengo la kuboresha maisha ya kila Mtanzania.

Mh. Pinda alisema Taarifa hizo ya Takwimu zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi si kwa ajili ya Serikali pekee bali zitasaidia taasisi,mashirika, jumuiya na hata wananachi wa kawaida katika kujipangia mipango yao ya maendeleo.

Mwenyekiti huyo wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 alizipongeza Ofisi za Taifa za Takwimu Tanzania na ile ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zilizochukuwa za kuendelea kukamilisha takwimu zinazotokana na sense ya mwaka 2012.

Akitoa shukrani Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Watanzania wa pande zote za Muungano wanajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 ikiwemo uimarishaji wa sekta ya takwimu nchini.

Balozi Seif alisema Watanzania pamona na Washirika wote wa Maendeleo wanaoendelea kuiunga mkono Tanzania wamejenga imani kubwa na Ofisi za Takwimu Ya Muungano na Ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ubora wa takwimu zinazotolewa na Ofisi hizo.

“ Ni jambo la faraja kubwa kukufahamisha kuwa nchi yetu imeendelea kuwa moja ya miongoni mwa nchi za Bara la Afrika zinazofanya Sensa za Watu na Makazi kwa mafanikio makubwa “. Alisema Balozi Seif.

Alieleza kwamba sifa hii kubwa imekuwa moja ya sababu na kivutio kwa Washirika wa Maendeleo kuendelea kuiunga mkono Tanzania mara kwa mara sio tu katika kufanya Sensa ya Watu na Makazi bali pia katika maeneo mengi ya ukusanyaji wa takwimu nchini.

Balozi Seif alifahamisha kwamba kwa kuwa yeye na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ni wasimamizi wa shughuli za Serikali watahakikisha kwa mba matumizi ya takwimu hizi na nyingine zinazotolewa na Ofisi husika yanapewa kipaumbele katika kupanga, kutekeleza na kutathmini programu na mipango mbali mbali ya Serikali na Taasisi zake katika ngazi zote.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Dr. Albina Chua akiwasilisha matokeo ya msingi ya chapisho hilo la Tatu la taarifa za msingi za Kidemografia,Kijamii na Kiuchumi alisema inapendeza kuona asilimia 40 ya viashiria vyote vilivyomo ndani ya malengo ya Milenia vimeanza kutumia Takwimu za Sensa ya watu na amakazi ya Mwaka 2012.

Dr. Albina alisema Serikali zilitoa miongozo kwa Taasisi za Fedha Nchini katika lengo la kuzijengea uwezo kaya zinazoongozwa na wanawake Nchini ambazo kwa mujibu wa Sensa hiyo zipo kaya Milioni 9,200,000 nchini Tanzania sawa na asilimia 33% zinazoongozwa na wanawake.

Kuhusu suala wa watu wanaojuwa kusoma na kuandika Dr. Albina Chua alifahamisha kwamba Takwimu za sensa zinaonyesha wazi kuwa asilimia 78% ya watu wenye umri kati ya miaka 10 hadi 15 kufikia mwaka 2012 wanaelewa kusoma na kuandika.

Utafiti huo kupitia zoezi la sense ya watu na amakazi ya mwaka 2012 umeonyesha wazi kwamba wanaume wamefikia asilimia 83% zaidi kuliko wanawake we nye asilimia 78%.

Naye kwa upande wake Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Hajat Amina Mrisho Said alisema chapicho hilo ni muendelezo wa machapisho mbali mbali yanayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania na ile ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hajat Amina alisema chapisho hilo litatoa viashiria tofauti kama kiwango cha uzazi, umri wa kuishi wa Mtanzania, vifo vya Watoto wachanga, kiwango cha vifo kwa Akina mama vitokanavyo na uzazi.

Alifahamisha kwamba hatua hiyo inakwenda sambamba na Taarifa nyengine kwa ajili ya kupanga mipango ya Maendeleo ya itakayozingatia mahitaji ya Taifa na wana jamii kwa jumla.

Kamishna huyo wa Sensa Tanzania alieleza kwamba matukio ya mchanganyiko wa mipaka baina y a wilaya,Mikoa na hata Vijiji zimeweza kuibuliwa kupitia zaoezi la Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Alisema Kamati hiyo inakusudia kushirikiana na Wizara inayohusika na masuala la ardhi katika kulirekebisha tatizo hilo ambalo linaweza kabisa kuondolewa kwa kutumia wataalamu wazalendo.

Akitoa salamu za shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha ina idadi ya watu { UNFPA }Bibi Maryam Khan alisema shirika hilo litaendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa n mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kupitia shirika hilo.

Bibi Maryam Khan alisema mkazo zaidi utaendelea kuwekwa katika kuona jamii kubwa ya watu duni hasa vijana na wanawake ambao ndio wengi wa wasimamizi wakubwa wa familia wanawezeshwa kiuchumi waweze kukabiliana na maisha duni katika maeneo yao.

Othman Khamis Ame
Ofisi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top