Chama cha Wananchi CUF leo kimeendelea na uchaguzi wake ngazi ya Wilaya kuwachagua viongozi mbali mbali wakiwemo Makatibu wa Wilaya, Wenyeviti pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu Taifa.

Viongozi wengine wanaochaguliwa ni wajumbe wa kamati tendaji pamoja na wajumbe wa viti maalum ngazi ya Wilaya.

Akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi Wilaya ya Magharibi unaofanyika ukumbi wa Basra Mtoni Kidatu, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Hamad Massoud Hamad, amesema viongozi wote watakaochaguliwa wana umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya chama hicho ngazi ya Taifa.

Hivyo amewataka wajumbe wa mkutano huo kuwa makini katika uchaguzi huo, ili kuwachagua viongozi watakao kuwa tayari kukitumikia chama, na kuepuka kuwachagua viongozi kwa sababu ya kujuana.

Amesema lengo la chaguzi hizo ni kuimarisha na kujenga chama kwa kufuata misingi ya demokrasia, na kuwasisitiza wajumbe hao kutochagua viongozi wenye makundi, misimamo ndani ya chama, na badala yake wachague viongozi majasiri na walio tayari kujitolea, ili kukiwezesha chama hicho kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mhe. Hamad Massoud ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Ole (CUF), ametanabahisha kuwa iwapo wajumbe wa mkutano huo watawachagua viongozi wasio kuwa na sifa, baraza kuu la uongozi linayo mamlaka ya kutengua uamuzi huo na kuitisha chaguzi nyengine.

Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, nae ameungana na wajumbe wa mkuano huo wa CUF Wilaya ya Magharibi, kuchagua viongozi wa Wilaya watakao kiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Uchaguzi huo unaendelea katika Wilaya za Magharibi, Kaskazini “B”, Kati na Kusini Unguja, baada ya kukamilika kwa chaguzi hizo katika Wilaya zote nne za Pemba na mbili za Unguja, hatua ambayo inakamilisha chaguzi hizo kwa Wilaya zote za Zanzibar.

Mchakato wa uchaguzi huo utaendelea kesho kwa wajumbe wa mkutano mkuu Taifa kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea kuchaguliwa katika baraza kuu la uongozi Taifa.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top