Na, Hassan Hamad (OMKR).

Wakati Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba akiichambua na kuikosoa bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015 kwa kueleza kuwa ina mapungufu mengi, ameunga mkono uamuzi wa Serikali kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa ya misamaha ya kodi kila robo ya mwaka kwa kuwatangaza walionufaika na misamaha hiyo kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari ofisi kuu za CUF Buguruni jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumba amesema utaratibu huo unaweza kusaidia kudhibiti misamaha ya kodi, na kuwawezesha wananchi kuwa na taarifa za misamaha na kuweza kudai kufutwa kwa misamaha hiyo.

Prof. Lipumba ambaye ni mchumi kitaaluma amesema ili kujenga utamaduni wa kulipa kodi kuwa ishara ya uzalendo ni muhimu misamaha ya kodi kwa viongozi wa serikali wakiwemo wabunge na mawaziri iondolewe, akifafanua kuwa ni vigumu kwa viongozi ambao hawalipi kodi kuwahamasisha wananchi kuwa wazalendo na kulipa kodi.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi chini ya viwango, Prof. Lipumba amesema kumekuwepo na tatizo la baadhi ya watendaji wa serikali kuchangamkia ununuzi wa vifaa kwa mategemeo ya kupata “Commission” kuliko malengo ya kuongeza ufanisi, jambo ambalo linapunguza ufanisi kwa miradi hiyo.

Aidha amepongeza utaratibu wa serikali wa kudhibiti matumizi ya umma kwa kuunganisha matumizi yote ya serikali chini ya mfumo mmoja unaosimamiwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali kupitia akaunti moja ya hazina “ Single Treasury Account”.

Amefahamisha kuwa kuwepo kwa utaratibu huo ni jambo zuri, lakini linahitaji maandalizi ikiwa ni pamoja na kufunga akaunti nyingi zinazotumiwa na taasisi nyengine za Serikali.

“Wizara na Idara nyingi zimeendelea kufungua akaunti mpya. Kuna Wizara zinazopinga Hazina kusimamia ulipaji wa makandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo. Utekelezaji wa ‘Single Treasury Account’ unahitaji kuungwa mkono kikamilifu na Rais”, alifafanua Prof. Lipumba.

Hata hivyo amesema bajeti hiyo bado haijatoa kipaumbele kwenye miradi ya maendeleo, na kwamba bajeti mbadala ilitakiwa ijikite katika ukusanyaji wa mapato kwa umakini, sambamba na kuwepo matumizi mazuri ya fedha za umma.

Aidha ameelezea haja ya kuwepo mikakati madhubuti ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotumia mali ghafi za ndani, na kuweza kuajiri watu wengi katika viwanda vya nguo na bidhaa nyengine za matumizi ya ndani.

0 comments:

 
Top