Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzia sasa haitachukuwa dhamana tena ya kulipa gharama zozote zitakazotokana na baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi mwao kwa kuvunjiana vyombo vyao wavyovitegemea katika kuendesha maisha yao ya kila siku. 

Alisema kitakachosimamiwa zaidi kwa sasa katika kukabiliana na wimbi hilo linaloonekana kuendelezwa katika baadhi ya maeneo hapa nchini ni kufuatwa kwa mkondo wa sheria dhidi ya watu watakaohusika na uharibifu wowote ule wa mali za raia au za Umma.

Balozi Seif alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kivunge kwenye uwanja wa michezo wa Good Hope Mkwajuni kufuatia tukio la kuchomwa moto kwa chombo cha uvuvi cha wanakijiji wa Kivunge kilichofanywa na wavuvi wa Kisiwa cha Tumbatu Tarehe 1 Januari mwaka 2014.

Alisema tabia hii ya migogoro ya wavuvi ambayo inaonekana pia kuongozwa na ushabiki wa kisiasa imekuwa ikiipa mzigo mkubwa Serikali Kuu kwa kulipa fidia masuala ambayo yanaweza kudhibitiwa na wahusika wa matukio hayo.

Balozi Seif alieleza kwamba masuala ya maendeleo na kiuchumi kuingizwa mambo ya kisiasa kamwe hayatekelezeki na daima wananchi wataendelea kuharibikiwa kimaisha.

Aliwataka wananchi wa Tumbatu na Kivunge kuendelea kushirikiana pamoja katika masuala ya maendeleo kwa vile ni ndugu wa damu. Lakini inapotokea hitilafu baina yao vikao vya pamoja katika kufafuta suluhu ya hitilafu hiyo ni jambo la msingi.

Alieleza kwamba uvuvi ni sekta kubwa ya uchumi inayopaswa kulinda wakati wote na kuwaomba wananchi walio wengi wa maeneo hayo kuepuka migongano isiyokuwa na sababu za msingi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wananchi hao kwamba Serikali inakubali kubeba mzigo wa kulipa gharama za vyombo vilivyoharibiwa katika mizozo hiyo lakini ikionya kuwa ni dhamana ya mwisho.

“ Likiwa ni tukio la mwisho kubebwa na Serikali tutalipa gharama za boti pamoja na vifaa vyake kwa kile chombo cha wavuvi wa Kivunge na Vifaa na mashine ya boti kwa kile chombo cha wavuvi wa Tumbatu. Nahitaji kupatiwa tathmini ya ghamama ya kile chombo cha Tumbatu “. Alifafanua Balozi Seif.

Akizungumzia suala la uhifadhi wa rasilmali za baharini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa wavuvi wote nchini kuendelea kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa na serikali katika hifadhi ya rasilmali hizo.

Hata hivyo Balozi Seif aliwatahadharisha baadhi ya wasimamizi wa rasilmali hizo kuacha tabia ya kujichukuliwa sheria mikononi mwao na badala yake wahusika wa uvunjifu wa taratibu hizo wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa hatua.

Mapema akitoa taarifa ya tukio hilo mwakilishi wa wananchi hao wa Kijiji cha Kivunge Bwana Sharifu Kombo Sharifu alisema wananchi hao waliomba kupatiwa chombo chao ili waendelee kuendesha maisha yao kama kawaida na kukabiliana na ukali wa maisha uliowazunguuka.

Bwana Sharifu kwa niaba ya wenzake wameiomba Serikali kupitia vyombo vyake vya sheria kuchukuwa hatua za haraka wakati yanapojitokeza matukio kama hayo ili kuepuka cheche za fitina zinazotumiwa na baadhi ya watu kuchochea migogoro kama hiyo wakati inapojitokeza kwenye maeneo mbali mbali nchini.

Wananchi hao wa Kijiji cha kivunge walieleza kwamba katika kujiepusha na uvuvi haramu hasa ule wa juya uliopigwa marufuku na taasisi zinazosimamia mazingira wameiomba Serikali kuu kuangalia uwezekano wa kuwapatia zana za kisasa za uvuvi ili kuondokana na uvuvi huo haramu.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pembe Juma Khamis alisema Serikali ya Mkoa huo ilichukuwa hatua mara moja kukabiliana na mzozo uliojitokeza kati ya wavuvi wa Tumbatu na Kivunge kufuatia chombo cha uvuvi cha Kivunje kuchomwa moto Kisiwani Tumbatu.

Mh. Pemba alisema juhudi hizo zilipelekea Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Shein kuunda kamati iliyoshirikisha wahusika wa pande zote mbili zilizozozana ikijumuisha pia maafisa wa ulinzi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akiwaomba kuendelea kuwa wastahamilivu wananchi wa Kivunge Mh. Pembe alisema kamati hiyo pia inachunguza eneo lililowekwa hifadhi ya mazalio ya Samaki liliopo Kisiwa cha Tumbatu na hatua za kuwapatia fursa wavuvi kuendelea na kazi zao itachukuliwa bila ya kuathiri hifadhi hiyo.

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Haji Juma Haji aliwatahadharisha Wana CCM na Wananchi wa Kijiji hicho kuwa makini na cheche za uchochezi zinazoonekana kupenyezwa katika maeneo yao.

Ndugu Haji alisema mgogoro wa tukio hilo haukutoa haki kwa baadhi ya watu kukilaumu Chama cha Mapinduzi pekee kwa vile wahusika wote wa mzozo huo wana itikadi tofauti za Kisiasa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top