Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inafikiria kujenga Ukumbi Mkubwa wa Heshima ili ipate fursa zaidi ya kujitangaza katika Nyanja za Kimataifa Kiutalii.

Alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zimebarikiwa kuwa na mandhari nzuri sambamba na Rasilmali nyingi za kuvutia zinazoweza kutoa fursa kadhaa za kuongezeka kwa uchumi.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Ujumbe wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania { TAWJA } ukiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Jaji Engera Kileo hapo katika Hoteli ya Kimataifa ya Naura Spring Mjini Arusha.

Mazungumzo hayo yalifanyika mwishoni mwa Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } uliochukuwa siku Nne na kufanyika ndani ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha {AICC }.

Alisema Dunia inaelewa uzuri wa Tanzania Kiutalii na kimazingira jambo ambalo Serikali kwa kushirikiana na taasisi na jumuiya za kiraia zinapaswa kujiandaa mapema katika kujenga miundo mbinu itakayosaidia kuzitumia vizuri rasilmali hizo pamoja na mandhari zilizomo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alivipongeza Vyama vya Majaji Wanawake vya Dunia na Tanzania kwa uamuzi wao wa kuufanya Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ} kufanyika Nchini Tanzania.

Balozi Seif alisema Mkutano huo kwa kiasi kikubwa umesaidia kuongeza Uchumi na mapato ya Taifa kwa vile washiriki wa Mkutano huo wametumia fursa kubwa ya kutembelea maeneo ya historia pamoja na mbuga za Taifa.

Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania {TAWJA } Jaji Engera Kileo alisema Mkutano huo umeisaidia Tanzania kujitangaza vyema kiutalii, kiutamaduni na kimazingira.

Jaji Engera alisema wajumbe wa Mataifa 50 kati ya 100 wanachama wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } yaliyojumuisha washiriki wapatao 550 katika Mkutano huo wamevutiwa na hali ya mazingira ya Historia ya Tanzania.

Mwenyekiti huyo wa Chama cha Majaji wanawake Tanzania alieleza kwamba vikao vya Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } kimekuwa kikiendesha mikutano yake kila baada ya miaka miwili katika nchi mbali mbali wanachama.

Alisema Mkutano wa kwanza wa Chama hicho ulifanyika Nchini Argentina na huu wa Tanzania ni mara ya pili kufanyika Barani Afrika
ukitanguliwa na ule wa Uganda mwaka 2008.

Wajumbe wa Mkutano huo wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani walipata fursa ya kujumuika pamoja katika chakula cha usiku kilichondaliwa maalum kwa ajili ya kuagana baada ya kumaliza mkutano wao.

Tafrija hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Maunt Meru ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mh. Omar Othman Makungu.

Chakula hicho cha usiku kiliambatana na ngoma za Utamaduni kutoka Kikundi cha Jeshi la Kujenga Taifa { JKT } Kambi ya Oljoro pamoja na Muziki wa waimbaji mbali mbali ndani na nje ya Nchi ambapo Wajumbe hao walipata fursa ya kujimwaga vyema uwanjani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top