Serikali zote mbili nchini ziko makini katika kufuatilia vitendo vinavyoonekana kufanya au kuandaliwa na baadhi ya makundi vikiashiria matukio ya kihuni yanayosababisha wasi wasi miongoni mwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Wanachama wa chama cha Mapinduzi, wapenzi pamoja na Wananchi wa Jimbo la Nungwi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo wa skuli ya Nungwi Mkoa Kaskazini Unguja.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema jamii ilishuhudia matukio ya uvunjifu wa amani katika miezi ya hivi karibuni iliyolenga kuhujumu mali za Serikali, chama tawala cha ccm na hata baadhi ya mali za raia kwa visingizio visivyoeleweka.

“ Tunaposema hivi vikundi vya kihuni vina mkono wa Kisiasa hatusengenyi wala kuonea lakini ukweli uko wazi ni hujuma zinayofanywa na makundi hayo huelekezwa kwa mali za chama tawala na Serikali yake. Kwanini hatujashuhudia makundi hayo kuhujumu mali na ofisi za vyama vya upinzani ? “. Aliuliza Balozi Seif.

Aliwatahadharisha vijana wote nchini kujiepusha na ushawishi wa kujiingiza katika vikundi hivyo vinavyoonekana kuendesha mambo yao kwa kisingizio cha kutangaza Dini.

Akizungumzia siasa Balozi Seif alisema upinzani uliopo nchini Tanzania hadi hivi sasa bado haujaainisha nini wanataka katika mfumo wa Serikali ndani ya Mabadiliko ya Katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejitahidi kadri ya uwezo wake kutoa fursa pana kwa kila mwananchi kupitia Kamati iliyoundwa kukusanya maoni ili watoe maoni yao jinsi mfumo wanaoutaka, fursa ambayo hata upinzani ulishiriki kikamilifu kutoa mawazo na mapendekezo hao.

Balozi Seif aliendelea kuwanasihi wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba Tanzania kupitia upande wa Upinzani kurudi ndani ya vikao vya Bunge hilo Mwezi Agosti Mwaka huu ili kukamilisha jukumu walilokabidhiwa na Umma.

Alisema mfumo waliouchukuwa wa kuamua kutoka nje ya vikao na kuendesha mikutano ya hadhara katika maeneo mbali mbali ya nchi unawanyima haki wananchi waliowachagua kuitekeleza kazi waliyowapa.

“ Ukweli ulio wazi ni kwamba Katiba ya nchi kamwe haitungwi kwenye mikutano ya hadhara na mfumo wa Viongozi hao wa upinzani utawanyima haki yao ya msingi wananchi “. Alifafanua Balozi Seif.

Naye Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Mjini Zanzibar Mh. Salmin Awadh Salmin aliwaasa viongozi wa kidini kuacha kujiingiza katika masuala ya kisiasa ambayo yanaweza kuwachanganya waumini wanaowaongoza.

Mh. Salmin alisema hoja binafsi inayotajwa hivi sasa kupelekwa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi isiwe ndio sababu kwa baadhi ya viongozi hao kutafuta chanzo cha kuleta mtafakuri ndani ya jamii.

Mnadhimu huyo wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia CCM aliendelea kusisitiza kwamba hoja hiyo ya kuulizwa Wananchi wa Zanzibar kama bado wanaendelea kuridhika na mfumo uliopo wa uendeshaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar itawasilishwa kwenye vikao hivyo wakati ukifika.

“ Hoja kama hiyo binafsi iliwahi kuwasilishwa Barazani, ikajadiliwa na hatimae wananchi wakapewa fursa ya kupiga kura ya maoni na kuamua kuikubali kwa zaidi ya asilimia 60%. Kwanini sasa kuwe na wasi wasi kwa kwa kupelekwa tena hoja nyengine binafsi kama katiba ya Zanzibar inavyoelezea “. Alisema Mnadhimu huyo wa Baraza.

Alifahamisha kwamba kilichopo mbele hivi sasa ni kwa wananchi kuendelea na harakati zao za kimaisha kama kawaida, lakini itakapofikia wakati wa suala hilo wao ndio watakaoulizwa na kuamua endapo bado watapenda kuendelea kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar au la.

Katika Mkutano huo wa hadhara wa Jimbo la Nungwi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kuunga mkono sekta ya michezo walijitolea kuchangia Seti za jezi na mipira ya Soka na Netiboli kwa timu18 zilizomo ndani ya jimbo hilo.

Hata hivyo bado thamani halisi ya gharama za vifaa hivyo vya michezo bado haikufahamika.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top