Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Majaji Wanawake wana wajibu mkubwa wa kuvitumia vyombo vya Habari katika kutoa elimu kwa umma itakayosaidia kupunguza wimbi kubwa la unyanyasaji wa kijinsia ndani ya Jamii.

Alisema unyanyasaji huo wa kijinsia kwa kiasi kikubwa unaonekana kuwaandamana zaidi wanawake na watoto katika Mataifa mbali mbali duniani hasa kwa zile nchi change.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati akiufunga Mkutano wa siku Nne wa Kimataifa wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani {IAWJ } uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha {AICC }.

Alisema uelewa mkubwa miongoni mwa Jamii ndio msingi imara na sahihi unaochangia kupunguza matatizo makubwa yanayowakabili wananchi na hasa unyanyasaji wa Kijinsia, na hili hupatikana endapo Wana Taaluma wa fani mbali mbali na Jamii husika wanapoamua kuvitumia vyombo vya Habari katika kupashana elimu.

Aliwataka Majaji wanawake kushirikiana zaidi katika kutoa haki sawa kwa mshitakiwa na aliyedhalilishwa wakati wanaposhughulikia kesi mbali mbali hasa zile za uzalilishaji wa kijinsia.

“ Majaji wanawaketumekuwa tumeshuhudia wanavyofanya kazi nzuri wakati wanapotekeleza majukumu yao waliyopangiwa hasa zile kesi za udhalilishaji wa kijinsia ambazo huwakumba zaidi wanawake na watoto wadogo “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali wakati wote zinakuwa tayari kushirikiana na Taasisi na Wananchi katika kuona changamoto zinazozikabili jamii na kuleta athari zinapatiwa ufumbuzi.

Alisema unyanyasaji wa kijinsia unaoelekezwa zaidi kwa wanawake na watoto hivi sasa umeenea katika maeneo mbali mbali ya Dunia kiasi kwamba Wasimamizi wa sheria kwa kushirikiana na wananchi wanapaswa kushirikiana katika kupiga vita vitendo hivyo viovu.

Balozi Seif alitolea mfano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyojitahidi kutoa fursa kwa wanawake Vijana kujipatia elimu ndani ya kipindi cha miaka kumi sasa jambo ambalo limeleta mafanikio makubwa katika mpango wa Serikali wa kujenga usawa wa kijinsia katika masuala ya Uongozi.

“ Katika kuendeleza dhana nzima ya utawala bora na usawa wa Kijinsia Serikali imepandisha daraja la uwakilishi wa wanawake katika fani ya Sheria na tayari Majaji wanawake wamepandishwa daraja la kwanza katika Mahkama Kuu ya Zanzibar mwaka 2010 “. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } na ule wa Chama cha Majaji Wanawake cha Tanzania { TAWJA } kwa uamuzi wao wa pamoja wa kufanya Mikutano hiyo kila mwaka.

Alisema Mikutano hiyo ikiwa na maudhui ya Haki kwa wote { Justice for all } kwa kiasi kikubwa hutoa fursa ya kupanua wigo wa mawasiliano kati ya Majaji Wanawake Duniani ili kujenga mazingira bora ya uwajibikaji.

Alifahamisha kwamba mazingira hayo huiwezesha jamii iliyoelimika kupata nguvu za upatikanaji wa haki za msingi za kiraia, ukuzaji wa haki za binaadamu pamoja na kujenga uadilifu.

Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani Jaji Eusebia Munuo alisema Wanachama wa Chama hicho hushirikiana na Taasisi na vyama vyengine katika masuala ya upatikanaji wa haki, kutoa elimu kuhusiana na haki za Binaadamu na jinsi Wanawake wanavyoweza kupata huduma za Mahkama.

Jaji Munuo aliosema wanachama hao pia huendeleza Mtandao wa Kimataifa wa Majaji wanawake pamoja na kutengeneza fursa za kubadilishana uzoefu,Taaluma na kuchapisha vijarida kuhusu suala la Utawala wa Sheria.

Akitoa salamu Mwenyekikti wa Chama cha Majaji Wanawake wa Marekani { NAWJ USA } Jaji AnnaBlackburne – Rigsby amesema Vyama vya Majaji Wanawake sehemu mbali mbali Duniani vimechukizwa na kitendo cha Kundi la Boko Haramu Nchini Nigeria cha kuwatyeka wasichana wadogo wasiokuwa na hatia yoyote.

Jaji Anna alisema kitendo hicho mbali ya kuwadhalilisha wasichana hao karibu wiki kadhaa sasa lakini pia kinakwenda kinyume na haki za Binaadamu sambamba na kuwatia hofu wazazi wa watoto hao.

Wajumbe wa Mkutano huo walitoa Baraka za kufanyika kwa Mkutano wa 13 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani Mei mwaka 2016 utakaofanyika Mjini Washington Nchini Marekani ambao ndio chimbuko la Chama hicho.

Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania { TAWJA } Jaji Engera Kileo alimkabidhi Bendera Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake cha Marekani Jaji Anna Blackburne – Rigsby kama ishara ya kuwa mwenyeji wa Mkutano huo wa 2016 kitendo ambacho kilishabikiwa kwa nderemo na wajumbe wa Mkutano huo.

Wajumbe wa Mkutano huo kutoka Chama cha Majaji wanawake kutoka Nchini Philippines walitoa burdani ya aina yake wakati wakionyesha utamaduni wao ulioambatana na muziki maalum wa Nchi hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama chao Jaji Teresita Leonardo – De Castro.

Mkutano huo wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } ulifunguliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ukishirikisha wajumbe wasiopungua 550 kutoka Mataifa 50 kati ya 100 yaliyo wanachama wa Chama cha Majaji Duniani { IAWJ }.

Chama cha Majaji Wanawake Duniani kiliasisiwa mwaka 1991 Mjini Washington Nchini Marekani kikiwa na wanachama zaidi ya elfu Nne kutoka Mataifa tofauti Ulimwenguni.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top