Na: Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesisitiza diplomasia ya kiuchumi kwa mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi, ikiwa ni jitihada za kukuza na kuendeleza uchumi wa nchi.
Akizungumza na balozi wa Tanzania nchini Sweeden ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema suala la kukuza uchumi linapaswa kupewa umuhimu wa kipekee, na kwamba mabalozi wana nafasi kubwa ya kuitangaza Tanzania kiuchumi.
Amesema Sweeden ni miongoni mwa nchi zenye mahusiano ya karibu na Tanzania, hivyo balozi huyo ana jukumu la kuhakikisha kuwa uhusiano huo unakuzwa na kuendelezwa zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Sweeden ni mshirika wa karibu sana wa Tanzania na uhusiano wetu ni wa muda mrefu sana, hivyo nakuomba ufanye juhudi za makusudi kuendeleza uhusiano huo, ukiwemo pia uhusiano wa mashirikia ya misaada kama vile shirika la SIDA”, Maalim Seif alimueleza balozi huyo.
Mhe. Maalim Seif amesema Tanzania ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Sweeden katika kukuza uchumi wake, na kumtaka balozi huyo kutumia fursa hiyo kuitangaza Tanzania katika sekta za kiuchumi ikiwemo utalii.
Amefahamisha kuwa Tanzania ina vivutio vingi vya utalii kwa pande zote mbili za Muungano, na iwapo vivutio hivyo vitatangazwa vizuri idadi ya watalii itaongezeka kwa kasi kubwa na kusababisha uchumi wa nchi kukua kwa kasi.
Amesema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla inaweza kutumia uzoefu wa nchi hiyo katika kukabiliana na masuala mtambuka yakiwemo mazingira, watu wenye ulemavu, dawa za kulevya, Ukimwi na mabadiliko ya tabia nchi.
Nae Balozi huyo mpya wa Tanzania nchini Sweeden balozi Dorn Msechu, amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa atafanya kazi kwa kadri ya uwezo wake kuhakikisha kuwa mahusiano ya kiuchumi baina ya Tanzania na Sweeden yanaimarika.
0 comments:
Post a Comment