Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema uwekezaji wa hoteli za kisasa zenye hadhi ya Kimataifa, utaisaidia Zanzibar kujitangaza kiutalii, na kuwafanya watalii wa hadhi ya juu pamoja na viongozi wa kimataifa kushawishika kuja kuitembelea Zanzibar.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati akitembelea mradi wa ujenzi wa hoteli ya kisasa ya Grand Hyatt unaotekelezwa na Kampuni ya Dubai katika eneo la Shangani, mkabala na jengo la Mambo msige mjini Zanzibar.

Amesema kwa kipindi kirefu Zanzibar imekua na upungufu wa Hoteli zenye hadhi ya kimataifa, na kwamba kukamilika kwa ujenzi huo itakuwa faraja kwa Zanzibar, hatua ambayo pia itahamasisha wawekezaji wengine katika sekta mbali mbali za kiuchumi.

Katika ziara hiyo Mhe. Maalim Seif ameongozana na viongozi mbali mbali wakiwemo Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Mhe. Ramadhan Abdallah Shaaban pamoja na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na ujenzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mkongwe Bw. Issa Sarboko Makarani amesema ujenzi huo umezingatia viwango vya Kimataifa na umeridhiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu na shirika hilo linalojishughulisha pia na urithi wa Kimataifa, ambapo Mji Mkongwe za Zanzibar ni sehemu ya urithi huo.

Amesema hoteli hiyo itakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu, itakuwa na uwezo wa kuwahudumia watalii wa hadhi ya juu pamoja na viongozi mashuhuri wa kimataifa wakiwemo Marais.

Bw. Makarani amefahamisha kuwa hoteli hiyo ya kisasa ambayo itakuwa na maegesho yaliyo chini ya jengo hilo (underground parking), itakuwa hoteli ya kwanza ya aina yake kuwahi kujengwa Zanzibar.

Ujenzi wa hoteli hiyo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, unatarajiwa kugharimu dola milioni 35 za kimarekani, ambapo ujenzi wake tayari umefikia zaidi ya asilimia 90.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top