Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema uamuzi uliochukuliwa na Vijana wa CCM wa Kijiji cha Kidoti Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja wa kujiunga na darasa la Itikadi ndio njia ya msingi itakayowapa fursa Vijana hao kuielewa vyema historia ya Taifa hili pamoja na Chama chao.

Alisema ipo mikakati ya makusudi na ya muda mrefu iliyoandaliwa na watu wakiwemo baadhi ya wanasiasa ya kujaribu kuupotosha ukweli halisi wa Historia ya Taifa hasa Mpinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyolenga kuwakomboa wakwezi na wakulima wa Visiwa vya Zanzibar.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akisalimiana na Vijana wa Darasa la Itikadi wa Kijiji cha kidoti akiwa pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama Tawala cha CCM walioamua kufanya ziara maalum ya Chama ndani ya mkoa wa Kaskazini unguja kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.

Alisema wananchi walio wengi hapa Zanzibar ndani ya utawala wa kikoloni kwa zaidi ya karne mbili kabla ya Mapinduzi walikuwa wakikandamizwa, kudhalilishwa pamoja na kunyimwa haki zao za kimsingi madhila ambayo waasisi wa Taifa hili wakajipanga kukabiliana nayo kwa kufanya Mapinduzi.

Balozi Seif alifahamisha kwamba hadi sasa wapo watu wanaojaribu kufumbia macho ukweli huu na badala yake kujaribu kueneza kasumba mbaya dhidi ya mapinduzi ya Zanzibar ambayo ndio yaliyochangia kuzaliwa kwa Muungano wa Tanzania ambao kila Mtanzania anafaidika nao Kiuchumi, kisiasa na Kijamii.

“ Nakupongezeni sana Vijana kwa uamuzi wenu wa kujifunza Historia ya Chama chenu pamoja na Taifa hili kwa ujumla na huu ndio uzalendo halisi mnaopaswa kuujenga nyinyi viongozi wa kesho. Naomba muelewe kwamba mtu asiyejua historia yake ajitambue kuwa ni sawa na Mtumwa “. Alitanabahisha Balozi Seif.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwatanabahisha Vijana hao 80 wa CCM wa Darasa la Itikadi Kidoti kwamba Historia ya Zanzibar ilichafuliwa na baadhi ya watu kwa kujaribu kuvuruga mfumo wa Mitaala ya Elimu lengo likiwa kuondosha kwa makusudi somo la Historia katika maskuli hapa Zanzibar.

Katika kudhibiti mfumo na kudumishwa kwa historia ya Taifa hili Balozi Seif aliwaomba Wananchi wote nchini kuendelea kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi katika sera yake ya mfumo wa Tanzania kuendelea kuwa wa Serikali mbili ili kulinda Historia hiyo.

“ Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuunga mkono mfumo wa Serikali mbili na huu ndio msimamo wake hata katika Mkutano wa Bunge Maalum la Katiba Tanzania litakaloendelea tena na kikao chake baadaye mwezi Agosti mwaka huu baada ya kumalizika kwa Vikao vya Bunge la Bajeti na Baraza la Wawakikishi Zanzibar “ Alisisitiza Balozi Seif.

Alifafanua kwamba mikutano ya viongozi wa upinzani nje ya Bunge Maalum la Katiba ambalo ndio halali na kulazimisha rasimu ya katiba isibadilishwe ni upotoshaji wa kamusudi wa wananchi sambamba na ifinyu wa hoja zisizo na mantiki.

Katika kuunga mkono mikakati ya vijana hao wa Darasa la Itikadi la Kijiji cha Kidoti ya kujitafutia kipato na kukabiliana na maisha yao ya kila siku Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif aliwaahidi Vijana hao kuwachangia Vyarahani Vitano ili waelekeze nguvu zao katika kazi za amali.

Nao Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi walioambatana na Balozi Seif katika ziara hiyo ya kuimarisha Chama walikubali kuchangia shilingi Laki mbili ili kuwapa motisha vijana hao wa darasa la Itikadi la Kidoti.

Mapema katika Risala yao Vijana hao 80 iliyosomwa na mmoja kati yao Mwajuma Juma Haji waliwapongeza Wabunge na Wawakilishi hao wa CCM kwa umahiri wao wa kutetea msimamo wa CCM wa Serikali mbili ndani ya Vikao vya Bunge Maalum la Katiba Mjini Dodoma.

Vijana hao walielezea faraja yao kuona hakukuwa na Mbunge au Mwakilishi wa Chama chao aliyeonyesha msimamo wa kigugumizi katika kuutetea msimamo wao huo kwa pamoja.

Pia waliupongeza Uongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Wilaya na Mkoa wao kwa jitihada uliochukuwa wa kuwapatia makada wa kuwasomesha Historia ya Chama chao.

Hata hivyo Vijana hao 80 wa Darasa la Itikadi la Kijiji cha Kidoti waliuomba uongozi wa Juu wa Chama chao kuwafanyia utaratibu maalum wa ziara za kimasomo za kujifunza kivitendo badala ya kumaliza mafunzo yao ya nadharia.

Darasa hilo la Itikadi la Vijana hao wa CCM wa Kijiji cha Kidoti limeanza tokea Tarehe 20 mwezi wa Aprili mwaka 2013 na limekuwa likiendelea kwa kila Jumamosi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top