Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema Watanzania wana kila sababu ya kusherehekea miaka 50 ya Muungano kutokana na mafanikio yaliyopatikana.

Ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja kuimarika kwa hali ya usalama, ushirikiano na maelewano kwa wananchi wa pande mbili za Muungano.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika hafla ya mkesha wa miaka 50 ya Muungano ilivyofanyika viwanja vya Mnazimmoja jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda.

Amesema miaka 50 tangu kuasisiwa kwa Muungano huo ni kipindi kirefu cha kujivunia, ikilinganishwa kuwa nchi nyingi za Afrika zilizojaribu kuungana zimeshindwa baada ya kipindi kifupi cha miungano yao.

Hata hivyo amesema Muungano wa Tanzania bado unakabiliwa na kero nyingi zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi kwa maslahi ya pande zote mbili na vizazi vijavyo.

Hafla hiyo iliyoambatana na urushaji wa fashifashi, ilihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi.

0 comments:

 
Top