Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wana wajibu wa kutekeleza kazi zao kwa mujibu wa Kanuni walizojiwekea za kuendesha Bunge hilo ili kiuwa mfano mwema wa matendo mazuri mbele ya jamii ya Watanzani kutokana na dhima waliyokabidhiwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na wana Habari mbali mbali wanaoripoti matukio ya Bunge la Katiba hapo katika Ukumbi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mjini Dodoma.

Balozi Seif alisema vitendo vya uvunjifu wa amani kila siku ili Bunge Maalum la Katiba liahirishwe kwa sababu za Kisiasa na msimamo ya kisiasa inayofanywa na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo si jambo jema.

Alisema mchakato huo wa Bunge Maalum la Katiba umekuwa ukishuhudiwa na Wananachi walio wengi Nchini kutawaliwa na wanasiasa wanaoonyesha dhahiri nia zao za kutaka kuvunja Muungano kutokana na kauli zao.

Alieleza kwamba kaulio nyingi zinazotolewa na kushuhudiwa na Wananchi kupitia vyombo vya Habari zimekuwa na muelekeo wwenye kuchionganisha Wananchi wa pande mbili za Muungano.

“ Inasikitisha sana kuona baadhi ya wabunge wa Bunge la Katiba wanaendeleza ushabiki wa Kisiasa ndani ya Vikao vya Bunge hilo kwa kutengeneza mbinu za kuongeza muda wa Vikao wakisahau kwamba kodi za Wananchi zinapotea bila ya kufanya kazi zilizokusudiwa kufanywa na Waheshimiwa sisi Wajumbe “. Alisema Balozi Seif.

Balozi Seif alifahamisha kwamba pamoja na hatua nzuri iliyofikiwa na Wajumbe wa Bunge hilo ya kujadili Rasimu ya Katiba na kuweza kubadilisha, kuboresha, kuongeza au kupunguza lakini bado zipo changamoto zinazolikabili Bunge hilo.

Alizitaja baadhi ya change moto hizo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa uvumilivu miongoni mwa Wajumbne wa Bunge Maalum, Bunge kutawaliwa na hisia za kisiasa zaidi badala ya kuweka maslahi ya Taifa mbele pamoja na kuwepo kwa vikundi vya watu wachache wasiotaka mchakato huo wa Katiba Mpya kuendelea kutokana na utashi wa kisiasa.

Akizungumzia suala la Mikutano ya hadhara inayoanza kuchukuwa sura mpya ya kutaka kugawanywa Wananchi ndani ya kipindi hichi cha mchakato wa Bunge la Katiba Balozi Seif aliwatahadharisha Wananchi kuwa macho na tabia hizi zinazoonekana kutaka kuleta mgawanyiko wa Jamii kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kauli za Baadhi ya Viongozi wa Kisiasa kuwataka Wananchi wa Upande mmoja wa Muungano kuacha shughuli zao za Kimaisha na kurudi katika makazi yao waliyozaliwa ni kuashiria jinsi viongozi hao walivyo na nia mbaya katika kuvunja Umoja wa Nchi na Muungano uliopo hivi sasa.

Balozi Seif alieleza matumaini yake kwamba Muungano uliopo hivi sasa wa Tanzania itaendelea kudumu, kuwepo na kuendelea kwa kipindi kirefu kijacho kwa vile bado unaridhiwa na kukubalika na jamii ya wananchi walio wengi ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Uongozi wake kwa kazi waliyoifanya ya kukusanya maoni ya Wananchi pamoja na kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Dr Ali Mohd Shein kwa muongozo wao wa muelekeo wa mchakato huo.

Alisema dhamira ya Viongozi hao iko wazi na dhati katika kuhakikisha Taifa hili la Tanzania linapata katiba Bora ya Wananchi kupitia Bunge Maalum la Katiba lililoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83, toleo la Mwaka 2012.

“ Kazi iliyopo mbele yetu ni Bunge Maalum kukaa kama Kamati ambazo ni 12 ili kujadili kwa kina rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kupata Rasimu nzuri itakayoleta faida kwa Wananchi “. Alifafanua Balozi Seif.

Balozi Seif Ali Iddi aliwashukuru watendaji wa vyombo mbali mbali vya Habari kwa kazi nzito wanayoendelea kuifanya katika kuwapatia Taaluma na Habari Wananchi juu ya masuala tofauti ikiwemo mchakato wa Katiba unaoendelea Mjini Dodoma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa Wanahabari hao kwamba ni vyema wakaelewa kuwa bado wanakabiliwa na dhima ya kuielimisha Jamii umuhimu wa kuichunga amani iliyopo hapa Nchini.

“ Napenda muelewe kwamba bado mna dhima ya kuielimisha jamii umuhimu wa kuichunga amani iliyopo Nchini “. Alisisitiza Balozi Seif.

Akijibu baadhi ya maswali ya wana Habari hao likiwemo lile linalodaiwa kwamba Zanzibar imevunja Katiba kwa kubadilisha baadhi ya vifungu vya sheria na ikiwemo Zanzibar kuitwa Nchi, Balozi Seif aliwatoa hofu wana habari hao kwamba Zanzibar kamwe haijavunja katiba kwa vile haina Utaifa.

Alisema Utaifa uliopo na unaoendelea kutumiwa na kujuilikana ni ule wa Utanzania akatolea mfano masuala ya Kimataifa yanashughulikiwa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“ Hebu nikuulizeni Nyinyi Waandishi mna kumbu kumbu yoyote mnayoijua au kuikumbuka kwamba kuna Balozi yeyote wa Zanzibar katika Mataifa ya Kigeni ? “. Aliuliza Balozi Seif.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top