Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba misingi ya ufundishaji wanafunzi Maskulini itaendelea kukosekana iwapo idadi kubwa ya Wanafunzi itapindukia kiwango kilichowekwa Kitaifa au Kimataifa.

Alisema idadi ya kawaida ya wanafunzi ndani ya darasa moja inahitajika kuwa watoto wasiozidi arubaini wakiwa na vikalio pamoja na vifaa vyote wanavyohitajika kuwa navyo wanafunzi hao darasani.

Balozi Seif alisema hayo mara baada ya kukabidhiwa na kuvizindua rasmi vyoo 18 vya Skuli za Kijitoupele za Msingi A na B pamoja na ile ya Sekondari hafla iliyofanyika katika Skuli hiyo na kuhudhuriwa na Wanafunzi, Walimu pamoja na Wazazi wa Wanafunzi wa Skuli hizo.

Balozi seif alisema msongamano wa watoto wengi Darasani mbali ya kwenda kinyume na mfumo, taratibu na maadili ya ufundishaji ndani ya darasa lakini pia unabebesha mzigo mkubwa walimu kuweza kuhudumia wanafunzi hao kwa wakati mmoja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Kijitoupele kwa uamuzi wao wa kukubali Wanafunzi wao kuhamishwa kwenda kupata taaluma skuli nyengine ili kupunguza msongamano mkubwa wa wanafunzi ndani ya Skuli hizo.

“ Walimu wetu wamekuwa wakiendelea kupata mzigo mkubwa kuwasomesha watoto wetu kutokana na wingi wa idadi yao darasani. Inasikitisha sana kuona Darasa moja la Skuli hii lina wastani wa wanafunzi 240 jambo ambalo pia ni hatari kwa afya ya wanafunzi wenyewe “. Alifafanua Balozi Seif.

Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuangalia maeneo mengine ya wazi ndani ya Wilaya ya Magharibi ili kutoa fursa ya ujenzi wa Skuli nyengine Mpya zitakazosaidia kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa maeneo hayo.

Balozi Seif aliwasihi Wanafunzi hao kuendelea kuvitunza vyema vyoo hivyo ili vidumu kwa muda mrefu pamoja na kuwakumbusha kupenda masomo yao kwa lengo la kushika nafasi za Uongozi na Taaluma kwa Taifa hili hapo baadaye.

“ Nawajibu wa kuwapongeza Walimu na Kamati ya Wazazi wa Skuli hii kwa juhudi zao za usimamizi mzuri wa wanafunzi wao na kupelekea kutoa wanafunzi wengi wanaofaulu vizuri kuingia katika skuli mbali mbali za Michepuo hapa Nchini “.

Akisoma Risala kwa niaba ya Wanafunzi, Walimu na Wazazi wa Skuli hizo Mwalimu Hidaya Haji Mkema alilipongeza Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa { UNICEF } kwa msaada wa vyoo hivyo ambavyo lilikuwa na uwezo wa kuvijenga Skuli nyengine.

Mwalimu Hidaya alisema Skuli za Kijitoupele bado zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi changamoto ambayo iko katika hatua ya kutafutiwa ufumbuzi wake ifikapo mwaka 2015.

Alisema uandikishaji wa wanafunzi wapya katika skuli hizo za Kijitoupele A na B umefikia idadi ya watoto 800 kwa mwaka kiasi ambacho ni kikubwa kupindukia mfumo na utaratibu uliowekwa wa sera ya Elimu.

Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto { UNICEF } Mwakilishi wa Shirika hilo hapa Zanzibar Bibi Francesca Morandini alisema watoto wana haki ya msingi ya kupata elimu inayoambatana na usafi wa mazingira.

Bibi Francesca alisema utafiti uliofanywa miaka mitatu iliyopita na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika suala la huduma za usafi wa mazingira maskulini umethibitisha hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 300 kwa mwaka.

Mwakilishi huyo wa Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa hapa Zanzibar alieleza kwamba Taasisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar tayari wameshatengeneza muongozo wa ujenzi wa vyoo katika maskuli mbali mbali unguja na Pemba.

Alisema muongozo huo una lengo la kuwajengea mazingira rafiki wanafunzi na tayari umeshazinufaisha skuli nane za Pemba naTano kwa Unguja wakati awamu ijayo itahusisha skuli nyengine Sita hapa Zanzibar.

Naye kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar { WEMA } Bibi Mwanaid Saleh alisema mradi huo uliohusisha Skuli 13 Unguja na Pemba kwa ufadhili wa Unicef umegharimu Shilingi za Kitanzania Milioni Mia Tatu na Ishirini na Tano { 325,000,000/- }.

Katibu Mkuu Mwanaidi alizitaja Skuli zilizofaidika na mradi huo kuwa ni pamoja na Makombeni, Vitongoji, Wingwi,Kwale,Pujini, Mabatini na Konde kwa Pemba na Kijitoupele, Nyerere Msingi,Tunguu, Bububu na Mtopepo kwa Unguja.

Akimkaribisha Balozi Seif katika hafla hiyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna alisema Madarasa 40 yanahitajika kujengwa ndani ya Wilaya ya Magharibi ili kukidhi mahitaji yaliyopo ndani ya Wilaya hiyo.

Waziri Shamhuna alifafanua kwamba upo mradi maalum wa ujenzi wa Skuli kumi za Sekondari katika Wilaya zote za Zanzibar mradi ambao utatoa upendeleo wa kwanza kwa wilaya ya Magharibi ili kukabiliana na tatizo la msongamano wa wanafunzi katika Skuli za Wilaya hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top