Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuungua kwa studio za Radio Noor Fm, ni pigo kwa waislamu wa Zanzibar na Taifa kwa ujumla.

Amesema kituo hicho ni muhimu katika kutoa taaluma mbali mbali zikiwemo zile zinazohusiana na maadili ya kiislamu, jambo ambalo pia linaisaidia serikali katika kurejesha maadili mema kwa jamii.

Mhe. Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati akitembelea studia hizo zilizoko katika jengo la msikiti wa “Masjid Sahaba”, Mtoni Kidatu.

Amesema Radio hiyo imekuwa ikitoa fursa kwa masheikh na wanataaluma kuweza kusambaza taaluma hizo kwa jamii, na kwamba wananchi wamekuwa wakijifunza na kunufaika kutokana na matangazo yake.

Ametoa pole kwa uongozi wa Radio hiyo na wasikilizaji wote wa Radio Noor, kutokana na kuungua kwa radio hiyo, na hatimaye kukosekana kwa matangazo yake.

Mhe. Maalim Seif ametoa wito kwa waislamu wenye uwezo kuichangia radio hiyo ili iweze kurejesha matangazo yake kwa haraka, ambapo yeye ameahidi kuchangia shilingi milioni tano kwa ajili ya kusaidia kurejeshwa kwa huduma hiyo ya matangazo.

Nae Mkurugenzi wa Radio hiyo Sheikh Mohd Suleiman, amesema tukio hilo ni mfululizo wa matukio kadhaa ya aina hiyo yaliyowahi kukikumba kituo hicho tangu kilipoanzishwa miaka mitano iliyopita.

Amesema tukio hilo lililotokea usiku wa tarehe 09 mwezi huu, limepelekea kuungua kwa studio za kurushia matangazo pamoja na vitendea kazi vyake vinavyokisiwa kugharimu shilingi milioni themanini (80).

Wakati huo huo Maalim Seif amemtembelea mtangazaji wa Radio hiyo aliyelazwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ustadh Aboubakar Fakih ambaye alijeruhiwa baada ya kujitupa kutoka ghorofa ya pili, pamoja na kuwajuilia hali wagonjwa wengine waliolazwa katika wodi hiyo.

Kwa mujibu wa daktari wa zamu wa hospitali hiyo dokta Said Omar, mgonjwa huyo ambaye amepata majeruhi katika miguu yake yote miwili pamoja na mkono wa kulia, hali yake inaendelea vizuri.
Hata hivyo amesema atalazimika kubakia hospitalini hapo kwa kipindi kisichopungua miezi miwili, na kuelezea matumaini makubwa na kuweza kupoa na kuendelea na shughuli zake.

Hassan Hamad (OMKR)

0 comments:

 
Top