Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 inatarajia kuzindua Chapisho la Tatu la Taarifa za msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi Tarehe 23 April mwak huu wa 2014 katika kusherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tannganyika na Zanzibar.

Uzinduzi huo unaotarajiwa kufanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete utafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Mjini Dar es salaam.

Taarifa ya uzinduzi huo imefahamika ndani ya Kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kilichofanyika chini ya Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye ukumbi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iliyopo Mjini Dodoma.

Akitoa Taarifa ya Wizara ya Fedha ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mh. Muigulu Nchemba alisema maandalizi ya machapisho mengine 10 yanaendelea kufuatia kukamilika kwa zoezi la Sensa ya Watu lililofanyika mwezi Oktoba mwaka 2012 Nchini kote Tanzania.

Mh. Nchemba aliyataja baadhi ya machapisho hayo yatazingatia zaidi takwimu zilizokusanywa na wataalamu wa Sensa zinazohusu Vizazi na ndoa, Elimu, Uhamiaji na Makazi pamoja na hali ya ulemavu.

Alizipongeza Taasisi na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa kupitia Walaamu wao kwa kushirikiana na Wizara hiyo katika kufanikisha kazi ya Sensa licha ya changamoto kubwa za upatikanaji wa fedha.
“ Tunawashukuru wadau wetu wa maendeleo ambao kwa kweli wametusaidia kutuunga mkono katika zoezi hilo na zaidi ya Shilindi Bilioni Tatu {3,000,000,000 } walizitenga kwa ajili ya kazi hiyo “. Alisema Mh. Muigulu Nchemba.

Akitoa Taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi ya uhakiki wa Baadhi ya mipaka ya Wilaya Tanzania Bara na Zanzibar kwenye Kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa yaTakwimu Tanzania Dr. Albina Chua alisema zoezi la uhakiki huo tayari limeshafanyika kwa Wilaya za Gairo na Chemba kwa Tanzania Bara na Wete na Micheweni kwa upande wa Zanzibar.

Dr. Albina alisema uhakiki huo wa mipaka ya Wilaya na Halmashauri umekuja kufuatia mapungufu yaliyojitokeza katika baadhi ya Wilaya hizo na kusababisha kuwemo kwa matumizi ya mipaka zaidi ya mmoja.

Alisema Utekelezaji wa kazi hiyo ulitokana na matokeo ya kazi ya awali iliyofanywa katika Wilaya ya Gairo ambapo Kamati ya Taifa ya ushauri ya Sensa iliagiza kufanyika kama sampuli ya kujua tatizo la utoaji wa mipaka ya kiutawala.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mohd Hafidh akitoa Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi hiyo ya uhakiki wa mipaka kwa upande wa Zanzibar alisema kazi hiyo imeanza kwa kuundwa kwa Timu ya Maofisa watakaoshughulikia kazi hiyo.

Alisema kazi hiyo iliyoanza Tarehe 8 Aprili mwaka huu inatyarajiwa kuchukuwa wiki mbili katika Wilaya ya Wete na kuendelea katika Wilaya ya Micheweni lengo ni kuziwezesha Taasisi husika kujua changamoto mbali mbali za mipaka ya Wilaya na namna ya kuzitafutia ufumbuzi ili kuwa na Mipaka inayofanana.

Akitoa shukrani zake kwa Wajumbe wa Kamati hiyo Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Sekreteri ya Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa kwa Kazi kubwa inayoendelea kuifanya tokea kumalizika kwa zoezi la Sensa ya watu na Makazi Nchini Tanzania.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top