Ushirikiano unaoendelea kuonekana Kwenye miradi kadhaa ya maendeleo inayofanywa kwa pamoja kati ya wananchi na wawekezaji ni miongoni mwa mapenzi yaliyopo baina ya pande hizo mbili zikilenga zaidi katika kuimarisha uchumi na ustawi wa Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya kukifunguwa Kituo cha Huduma za Wajawazito kilichopo pacha na Kituo cha Afya Cha Pwani Mchangani Wilaya ya Kaskazini “A”, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kituo hicho cha huduma za wajawazito kikiwa ni vifaa vyote muhimu vya akina mama wajawazito kimejengwa kwa ufadhili wa Muwekezaji wa Hoteli ya Waride Resort kwa gharama ya shilingi Milioni 500,000,000/- wakati kile ya Afya ambacho tayari kimeanza kutoa huduma kimepata ufadhili wa Muwekezaji wa Ocean Paradise zote za Pwani Mchangani kwa gharama ya Shilingi Milioni 400,000,000/-.

Balozi Seif alisema wakati wafadhili na wawekezaji tayari wameshaonyesha muelekeo hamu kubwa ya kusaidia maendeleo ya wananchi wa maeneo wanayoekeza Wananchi wenyewe wana wajibu wa kuitunza miradi hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwapa nguvu zaidi wawekezaji hao kuendelea kusaidia kuunga mkono harakati za wananchi hao katika kujiletea maendeleo yao pamoja na kustawisha maisha yao ya kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Hoteli ya Waride Resort na ule wa Ocean Paradise kupitia muwakilishi wao Bwana Massimiliano Bramucci kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuipatia huduma za Afya Jamii katika masafa yasiozidi kilomita tano.

“ Nimefarajika na hatua zenu mlizozichukuwa za kusaidia maendeleo ya Wananchi wetu hasa katika Miradi ya Afya na Elimu jambpo ambalo umeipunguzia mzigo mkubwa Wizara yetu ya Afya ya kuendelea kusimamia masuala ya afya hapa Nchini “. Alifafanua Balozi Seif.

Akizungumzia huduma za Afya Balozi Seif aliwaasa wananchi kuendelea kuvitumia vituo vya afya kwa kuangalia afya zao na kuachana na kutumia dawa za miti shamba zisizo na kiwango ambazo kwa kiasi kikubwa huleta madhara kwa watumiaji hao.

“ Umefika wakati sasa ndugu wananchi wenzangu kuachana na dawa za kienyeji za miti shamba ambazo hazina kiwango ma rana nyingi huleta athari katika miili yetu “. Alisisitiza Balozi Seif.

Mapema Mwakilishi wa Hoteli ya Waride Resort Bwana Massimiliano Bramucci ambaye ndie mfadhi ya Kituo hicho cha huduma za Waja wazito Pwani Mchangani amewashukuru wananchi wa Pwani Mchangani kwa ushirikiano wao uliosaidia kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati.

Bwana Massimiliano katika kushajiisha wananchi hao kuvitumia Vituo hivyo kwa kupata huduma za afya ameahidi kufanya sherehe kubwa kwa motto wa mwanzo atakayezaliwa katika Kituo hicho cha huduma za wajawazito cha Pwani Mchangani.

Akitoa salamu za Wizara ya Afya Zanzibar Kaimu Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dr. Jamala Adam alisema ujenzi wa vituo hivyo viwili ni mfano mzuri wa mashirikiano kati ya wananchi wa Pwani Mchangani na Wawekezaji.

Dr. Jamala alisema ijenzi wa Vituo hivyo unakwenda sambamba na ile azma ya Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kutangaza huduma za Afya kutolewa bure kwa wananchi wote mnamo mwaka 1965.

Katika Risala yao Wananchi hao wa Kijiji cha Pwani Mchangani iliyosomwa kwa niaba yao na Mwalimu Mwinyi Sauti Haji aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia mafunzo ya Afya Vijana wa Kijiji hicho ili waje kusaidia kutoa huduma hapo baadaye katika Vituo hivyo.

Mwalimu Mwinyi Sauti Haji aliushukuru Uongozi wa Hoteli ya Waride Resort na ule wa Ocean Paradise kwa misaada yao mikubwa ya maendeleo ambayo inakwenda sambamba na malengo ya Milenia.

Kituo cha Huduma za Wajawazito cha Kijiji cha Pwani Mchangani pamoja na Kituo cha Afya viliopo Pacha vimefanikiwa kuwa na Vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa maradhi mbali mbali ikiwemo mashine ya Utra Sound, Chumbna cha Operesheni mdogo, Maabara pamoja na chumba cha kupumzikia wagonjwa.

Zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni mia Tisa zimetumika katika ujenzi wa Vituo vyote viwili ikiwa ni mchango uliogharamiwa na wafadhili wa Hoteli hizo mbili zilizomo ndani ya Kijiji cha Pwani Mchangani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top