Jamii nchini imetahadharishwa kuwa makini katika kipindi hichi kilichoanza cha msimu wa mvua za masika ambacho kimezoeleka kuwa na matukio mbali mbali ya maafa yanayoleta athari kwa wananachi.

Tahadhari hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiwafariji wananchi waliokumbwa na maafa kufuatia Upepo Mkali ulioambatana na mvua jana jioni katika maeneo ya Kwaalamsha, Makadara na Mkele ndani ya Wilaya ya Mjini.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mbali ya mvua na upepo lakini kipindi hichi cha masika pia hukumbwa na miripuko ya maradhi tofauti ya kuambukiza jambo ambalo jamii inapaswa kujihadhari nayo.

Aliwahakikishia wananchi hao kwamba Serikali Kuu kupitia Idara yake ya Maafa ambayo iko chini ya Ofisi yake inaendelea kufanya tathmini na hasara iliyowakumbwa wananchi hao na baadaye iangalie namna ya kusaidia nguvu zitakazowawezesha kurejea katika mazingira yao ya awali.

“ Nimekuja na Timu yangu Katibu Mkuu, Mkurugenzi Maafa na timu yake kuanza tathmini na maafa haya na baadaye kuandika ripoti itakayotusaidia sisi Serikalini namna ya kuchukuwa hatua za kukabiliana na maafa hayo yaliyojitokeza “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi mbali mbali waliojitolea nguvu, maarifa na hata hifadhi ya dharura kwa wenzao waliopatwa na maafa hayo kufuatia upepo huo wa ghafla.

Alisema kitendo hicho mbali ya kuleta faraja kwa waathirika hao pamoja na Serikali kwa jumla lakini pia kimeongeza upendo na kuimarisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa Wananchi hao.

“ Ukweli nimefarajika sana kusikia kwamba majirani zenu walikuwa pamoja na nyinyi muda wote wa tukio hili. Huu hasa ndio ujirani mwema unaotakiwa kuwemo ndani ya nyoyo za wanaadamu wakati wote “. Alifafanua Balozi Seif.

Wakitoa shukrani zao kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi baadhi ya wananchi hao walioathirika na upepo huo walielezea kufarajika kwao na hatua zilizochukuliwa na majirani zao katika kuwasaidia kukabiliana na maafa hayo.

Nyumba zipatazo Tatu katika Shehia ya Kwaalamsha, Tano Sheria ya Mkele na nyengine kadhaa ambazo bado idadi yake hajijajuilikana katika Shehia ya Makadara zimeathirika kutokana na upepo huo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top