Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema hakufurahishwa na baadhi ya kauli zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete alipokuwa akizindua Bunge Maalum la Katiba na ameamua kumwandikia barua kumueleza masikitiko yake. 

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha CUF katika viwanja vya Kibandamaiti, Mhe. Maalim Seif alisema, Rais Kikwete kama mkuu wan chi, hakupaswa kuingiza misimamo ya chama chake kwa vile Katiba inayoandikwa ni ya wananchi wote na sio wa chama maalum. 

Maalim Seif alisema Rais alitarajiwa angetoa hotuba ambayo inawanunganisha Watanzania wote, lakini kilichotokea alitoa kauli ambazo ni za ubaguzi ambazo ni za kujenga chuki dhidi ya watu fulani. 

Alisema kwa mfano Rais kueleza kuwa wananchi wa Pemba ndio watakaoathirika chini ya mfumo wa Serikali tatu kwa vile ndio wenye mashamba mengi ya Vitunguu katika maeneo ya Tanzania Bara ni kauli ya kujenga chuki, kwa vile sio watu kutoka Zanzibar peke yao wanaofanya shughuli zao Tanzania Bara. 

“Sikutarajia hata siku moja Rais Kikwete atafitinisha watu, … eti Wapemba watafukuzwa, lakini Tanzania Bara wapo Wakenya na hata Wachina wanafanya shughuli zao, kwanini iwe Wapemba tu”, alihoji Maalim Seif. 

Alisema baada ya hotuba hiyo ya Rais, na nia ya CCM kulazimisha mfumo wa serikali mbili, licha ya wananchi wengi kupinga, msimamo wake yeye na Wazanzibari walio wengi sasa unabaki kuwa ni Serikali ya Mkataba, kama walivyotaka kwenye maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. 

Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema ishara za kuwa CCM hakina nia ya wananchi kupata katiba safi na kulazimisha misimamo yao inaonekana wazi katika uendeshaji wa Bunge la Katiba. 

Alisema Mwenyekiti wa Bunge hilo kwa kushirikiana na wajumbe wa CCM wamekuwa wakitumia wingi wao kulazimisha hoja zao, pamoja na kuteua viongozi kutoka chama hicho ili kupitisha matakwa yao, hata kama hayana maslahi kwa wananchi walio wengi. 

Alieleza kuwa hata Tume zilizioundwa na Mwenyekiti Samuel Sitta ni za upendeleo ambao takriban wajumbe wote ni kutoka CCM.
 
“Wenyevitio wote ni kutoka CCM anayewakilisha makundi mengine ni Hamad Rashid, sita akamteua Profesa Lipumba aingie, Mnyamwezi yule yuko makini amekataa, tunampongeza sana Profesa Lipumba”, alisema. 

Aidha, alimpongeza Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe, Pandu Ameir Kificho kutokana na ujasiri na uwezo mkubwa aliouonesha alipokuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalum kwa kufanya kazi bila upendeleo. 

Maalim Seif alisema Mhe. Kificho alifanya kazi kubwa nzuri tena bila ya kuwa na kanuni, lakini mMwenyekiti Sitta ameonyesha udhaifu mkubwa wa kuendesha Bunge hilo. 

Na Khamis Haji (OMKR)

0 comments:

 
Top