Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu Tanzania Bw. Ludovick Utouh, amekutana na uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kujadiliana juu ya masuala ya fedha ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2012.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika ofisi kuu za CUF Buguruni, Bw. Ludovick amesema ni jambo la faraja kuona chama hicho kimeonesha njia kwa vyama vyengine, kikiwa cha mwanzo kukaguliwa na chombo hicho.

Bw. Ludovick ambaye aliongoza ujumbe wa ofisi ya Mdhibiti na Mkuguzi Mkuu wa hesabu, ameelezea kuridhishwa na muendelezo wa masuala ya fedha ndani ya chama hicho, na kuahidi kutoa ripoti kamili katika kipindi cha siku 21.

Kikao hicho pia kilimuhusisha Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.

Wakati huo huo Maalim Seif amefanya mahojiano na kampuni ya Global Publishers Limited ya Dar es Salaam, inayochapisha magazeti ya Uwazi, Champion, Risasi, Ijumaa na Amani.

Pamoja na mambo mengine kampuni hiyo ilitaka kujua juu maendeleo ya chama hicho, pamoja na mafanikio, changamoto na utendaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kuhusu maendeleo ya chama hicho Maalim Seif amesema chama hicho hakijafifia kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, na badala yake kimezidi kuimarika katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.

Amesema lengo kuu la chama cha siasa ni kushika hatamu za dola, na kwamba tayari chama hicho kimekuwa sehemu ya serikali katika serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Akipoulizwa kuhusu madai ya kukidhoofisha chama hicho kutokana na kushikilia wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akiwa pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif alisema kazi kubwa ya Katibu Mkuu ni kusimamia utekelezaji wa majukumu ya chama ambayo hufanywa na wasadizi wake wakiwezo naibu makatibu wakuu pamoja na wagurugenzi.

Hivyo amesema nafasi hiyo haiathiri ufanisi wa chama hicho, na kamwe haiwezi kuwa sababu ya kuzorotesha maendeleo ya chama, na kutoa mifano kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Dkt. Ali Mohd Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Maalim Seif pia alizungumzia juu ya suala la dawa za kulevya ambapo alisema ofisi yake ikiwa imepewa jukumu hilo, imekuwa ikipanga mikakati ya kila aina kuona kuwa tatizo hilo linadhibitiwa.

Hata hivyo amekiri kuwepo ugumu wa kukabiliana na tatizo hilo kutokana na jiografia ya Zanzibar ambayo imekuwa na njia nyingi zisizo rasmi, zinazofikiriwa kuingizwa dawa hizo ukitoa viwanja vya ndege na bandari zinazotambulika.

Amesisitiza haja kwa watendaji wa mamlaka za viwanja vya ndege na bandari kuwa waadilifu, na kuepukana na vishawishi vinavyoweza kupelekea uingizaji wa dawa za kulevya katika maeneo hayo.

Aidha amesema kwa sasa wamekuwa wakiweka udhibiti katika maeneo hayo yaliyo rasmi, pamoja na kusambaza elimu kwa vijana wakiwemo wanafunzi, juu ya athari ya dawa hizo.

Amehimiza mashirikiano baina ya vyombo vya dola na wananchi katika kukabiliana na tatizo hilo ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

“Tatizo hili halitomuathiri mtoto wa fulani tu bali tujue kuwa vijana wengi hata watoto wa viongozi na matajiri wanaathirika, kwa hivyo kitu cha msingi ni mashirikiano baina ya vyombo vyetu vya dola na wananchi”, alisisitiza Maalim Seif.

Hassan Hamad. (OMKR)

0 comments:

 
Top