Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi Wana Taaluma ya Maendeleo ya Jamii Nchini kuitumia vyema elimu yao katika kubadilisha maisha ya wananchi ili kufikia dhana halisi ya Maendeleo ya Jamii inayotoa nafasi kwa wananchi kujiunga kwenye vikundi vinavyolenga kutatua matatizo yao ya Kimaendeleo.

Alisema misingi ya dhana hii wakati wote inasisitiza kuwa maendeleo ya kweli ni ya watu na hapana budi kutokana na jitihada zao za hali na mali zinazopata msaada wa wataalamu wazalendo wa fani hiyo.

Balozi Seif alitoa nasaha hizo kwenye Mahafali ya Tatu ya wahitimu wa Shahada ya kwanza na Stashahada ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii mahafali iliyokwenda pamoja na Chuo hicho kuadhimisha kutimiza miaka 50 Tokea kuanzishwa kwake mwaka 1963 zilizofanyika kwenye chuo hicho kiliopo Tengeru Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.

Alisema itakuwa fedheha kubwa kwenye mitaa au Vijiji wanavyoishi wana taaluma hao wa Maendeleo ya Jamii kama kutakuwa na maradhi yanayoweza kuepukika, watoto wa mitaani,viwango vikubwa vya maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na mazingira machafu.

“ Kama mtashindwa kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo mnayoishi, mtawezaje kufanya hivyo kwa walio mbali nanyi ? Je kufanya hivyo kunahitaji usafiri na fedha za kujikimu ? ambazo tunajua wazi hazipatikani kukidhi mahitaji yote ya uendeshaji Serikalini ? Aliuliza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Sekta ya Maendeleo ya Jamii inapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa na sekta nyengine nchini katika kuleta mabadiliko ya maendeleo ya jamii kwa kutumia dhana hiyo ya Maendeleo ya Jamii.

Balozi Seis alisema Serikali iliamua kuweka mifumo tofauti ili kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo ambayo ilitumika kugharamia vifaa vya Viwandani vilivyohitajika katika utekelezaji wa miradi iliyobuniwa na kutekelezwa na wananchi hao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifafanua kwamba mbinu hii ya maendeleo ya jamii imeliwezesha Taifa la Tanzania kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwashirikisha wataalamu wa maendeleo ya Jamii.

Balozi Seif alitolea mfano wa mafanikio hayo yaliyopatikana katika sekta mbali mbali za Maendeleo na Kiuchumi hapa nchini kuwa ni pamoja na huduma za maji safi na salama, Afya bora, Elimu, lishe bora, Mali asili pamoja na Mazingira.

Aliwapongeza wahitimu waliozaliwa katika chuo hicho cha Maendeleo ya Jamii Tengeru katika miaka ya awali mara baada ya Uhuru ambao walifanya kazi kubwa kwa uzalendo, weledi na katika mazingira magumu bila ya kujali posho ya mazingira magumu.

Balozi Seif alielezea matumaini yake kwa wahitimu wapya waliomaliza mafunzo yao kwamba heshima hiyo ya wahitimu waliowatangulia wataienzi ili Taifa lipate kupiga hatua za haraka za maendeleo ikieleweka kuwa wao ni mhimili wa maendeleo ya kudumu hapa Nchini.

Akizungumzia kipindi cha miaka 50 tokea kuanzishwa kwa chuo hicho cha Maendeleo ya Jamii Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Mabibi na Mabwana Maendeleo waliopata taaluma kwenye chuo hicho kwa michango yao mikubwa ya Maendeleo kwenye sekta tofauti.

Alisema katika kipindi hicho ambacho ni kidogo kwa maisha ya chuo wataalamu wengi wa maendeleo ya Jamii wamezaliwa na kufanya kazi katika maeneo mbali mbali ya Taifa hili Mjini na Vijijini.

Mapema Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru Bwana Anatory Bunduki alisema chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1963 miaka miwili tu baada ya Uhuru kilianza na mafunzo ya cheti.

Bwana Bunduki alisema hivi sasa chuo hicho kimeshatoa wahitimu elfu 2,518 tokea kuanzishwa kwake na kwa wakati huu kishafikia ngazi ya shahada na Stashahada.

Alisema Mwaka 2000 chuo hicho kimetambuliwa rasmi na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kikiwa na lengo la kujitegemea chenyewe ambapo azimio la chuo hivi sasa liko kwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuliidhinisha rasmi.

Katika kukijengea uwezo zaidi wa utoaji wa Taaluma ya kisasa Mkuu huyo wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii alisema Uongozi wa Chuo hicho unaendelea na ujenzi wa Maktaba kubwa na ya Kisasa itakayowapa fursa wana taaluma wa chuo hicho kusoma Kitaalamu zaidi.

Hata hivyo Bwana Anatory Bunduki alifahamisha kwamba Chuo hicho bado kinakabiliwa na baadhi ya changamoto akizitaja kuwa ni pamoja na uchakavu wa miundo mbinu ya majengo, Kituo cha Afya pamoja na tatizo la usafiri kwa wanafunzi hasa wakati wanapokuwa kwenye mafunzo ya vitendo.

Akitoa Historia ya maadhimisho ya miaka 50 tokea kuanzishwa kwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Bibi Anna Maembe alisema wananchi wakiwezeshwa kitaaluma wana uwezo mkubwa wa kujiendesha kimaisha na kupiga hatua kubwa ya Maendeleo.

Kwenye mahafali hayo ya Tatu ya chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru Arumeru Arusha Wanafunzi 69 wamefaulu na kutunukiwa Shahada ya kwanza ya Maendeleo ya Jamii, usimamizi wa Programu za Maendeleo ya Jamii.

Vile vile Wanafunzi 55 wamefaulu na kutunukiwa Shahada ya kwanza ya Maendeleo ya Jamii, Upangaji wa uendeshaji miradi, wanafunzi 50 wamefaulu na kutunukiwa Shahada ya kwanza ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Maendeleo pamoja na wanafunzi Sita waliofaulu na kutunukiwa Stashahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top