Wakati Tanzania inakaribia kuingia kwenye uchaguzi Mkuu wa Tano mwakani unaoendelea kuhusisha mfumo wa vyama vingi vya Kisiasa tokea mwaka 1995 Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wametahadharishwa kujiepusha na tabia za vikundi miongoni mwao ambavyo vinaweza kupunguza nguvu za chama hicho katika dhana nzima ya kuendelea kushika dola.

Tahadhari hiyo imetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi wakati wa hafla fupi na kukabidhi mchango wa Mabati ya kuezekea 136 kati ya 236 yanayohitajika kutekeleza ahadi yake kwa Uongozi wa Tawi la CCM Mombasa kwa Mchina Wilaya ya Magharibi akiwa pia muanzilishi wa Tawi hilo.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema bado ana imani thabiti kwamba amani ya Taifa la Tanzania itaendelea kubakia ndani ya mikono ya Chama cha Mapinduzi kinachohubiri Umoja, Mshikamano na upendo miongoni mwa Wananachi wote.

“ Tusiichezee shilingi chooni akimaanisha kutahadharisha wanachama hao pamoja na Wananchi kuilinda amani ya nchi ambayo ndio muhimili wa jamii katika harakati za maendeleo “. Alisema Balozi Seif.

Alisema tabia ya makundi inayoonekana kujipenyeza ndani ya Chama hicho tokea uchaguzi wa mwaka 2010 ikiendelea kushikiwa bango na baadhi ya Viongozi inaweza kuijengea mazingira magumu CCM katika uchaguzi Mkuu ujao hapo Mwakani.

Alisisitiza umuhimu wa wanachama wa Chama cha Mapinduzi kuendelea kuimarisha Chama chao ili kusimamia vyema ilani na sera ya chama hicho iliyokubaliwa na Wananchi isimamie uendeshaji wa Serikali hapa Nchini.

Mjumbe huyo wa Kamakati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliupongeza Uongozi na Wanachama wa Tawi hilo kwa uamuzi wao wa kujenga Tawi lao jipya lenya hadhi inayokubalika na chama chenyewe.

Alisema Viongozi na Wanachama hao wametekele
za vyema maagizo ya Chama kwa kuwataka wanachama wake katika maendeo mbali mbali nchini kuendelea kujenga ofisi zenye kulingana na chama chenyewe.

“ Nimefurahi na kuridhika na ujenzi wa Tawi lenu zuri, kubwa na linalokwenda sambamba na hadhi ya chama chetu kinachosisitiza ujenzi wa matawi yenye kuimarisha pia uchumi utakaowasaidia kuendeshea shguhuli zao za kila siku “. Alifafanua Balozi Seif.

Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Tawi hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Tawi hilo ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Wilaya ya Dimani Ndugu Ahmada Abdullwakil alisema utashi wa wanachama wa Tawi hilo ndio uliopelekea maamuzi ya kujengwa kwa Ofisi hiyo.

Ndugu Ahmada alisema ujenzi wa Tawi hilo ulioanza Tarehe 1 Novemba 2013 utakakidhi mahitaji yote ya Ofisi kwa Wanachama hao ambao pia umezingatia uwepo wa ukumbi wa Mikutano utakaokuwa na uwezo wa kuchukuwa watu 150 kwa wakati mmoja.

Mapema Mwenyekiti wa Tawi la CCM la Kwa Mchina Mombasa Bibi Subira Kahalani alimpongeza Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi kwa jitihada zake za kuunga mkono ujenzi huo.

Bibi Subira Kahanani alisema uwamuzi wa Balozi Seif alioutoa Tarehe 1/11/2013 wa kuwataka wanachama na viongozi hao kujenga Tawi lao jipya ndio uliowapa hamasa wanachama hao wa kujenga tawi hilo.

Alifahamisha kwamba kukamilika kwa Ofisi hiyo kwa kiasi kikubwa kutawaondoshea shida na usumbufu wanachama hao wa sehemu ya kufanyia kazi zao ambapo walikuwa wakisumbuka kwa kipindi kirefu.

Ujenzi wa Ofisi hiyo ya Tawi la CCM Mombasa Kwamchina itakayokuwa pia na maduka Manne imeshafikia gharama ya shilingi Milioni Thalathini sadi hivi sasa ilipofikia hatua za Linta.

Wakati huo huo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akiambatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi amewasili Mkoani Dodoma kwa ajili ya kuhudhuria Kikao cha siku mbili cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Kikao hicho kinafanyika chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ambapo takriban wajumbe wote wa Kikao hicho wameshawasili tayari kuanza kwa kikao hicho.

Balozi Seif akiwa Mbunge wa Jimbo la Kitope na pia mjumbe wa Bunge la Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuungana na wajumbe wenzake kushiriki Vikao vya bunge hilo vinavyotarajiwa kuanza rasmi wiki ijayo.

Wajumbe wasiopunguwa mia sita wanatarajiwa kushiriki kwenye vikao hivyo miongoni mwao wakiwemo wale 201 walioteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwakilisha Taasisi na makundi tofauti ya Jamii hapa Nchini.

Bunge la Katiba linaanza baada ya kukamilika kwa mchakato wa kutoa maoni kupitia wananachi na baadaye mabaraza ya Katiba ya Wilaya kazi ambayo imekamilika na kupatikana kwa Rsimu ya Pili inayoratajiwa kujadiliwa na Wabunge hapo wa Bunge la Katiba.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top