Oman imeahidi kuendeleza mashirikiano yake na Zanzibar katika nyanja mbali mbali, ili kuimarisha uhusiano wa muda mrefu baina na nchi hizo mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi mpya wa Oman nchini Tanzania Sheikh Soud Ali Mohammed, wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ofisini kwake Migombani.

Balozi Soud ambaye alifika kwa ajili ya kujitambulisha, amesema Oman na Zanzibar zina uhusiano wa kindugu wa muda mrefu , na kuahidi kufanya kila liwezekanao kuona kuwa uhusiano huo unaimarika zaidi.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amemuhakikishia Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini mchango unaotolewa na Oman katika historia ya uhusiano baina yake na Zanzibar.

Amefahamisha kuwa Oman imekuwa ikitoa misaada kadhaa ya kijamii na kiuchumi kwa Zanzibar hasa katika Nyanja za elimu, afya na miundombinu.

Maalim Seif amesema Zanzibar imeanza kunufaika na nafasi za masomo nchini Oman kupitia ufadhili wa Mfuko wa Sultan Qaboos wa nchi hiyo, na kwamba hatua hiyo itaisaidia Zanzibar kuweza kufikia malengo yake.

Ametaja maeneo mengine ambayo Oman ilichangia kufanikiwa kwake kuwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa njia za kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, pamoja na kuchangia ujenzi wa Chuo cha Afya.

Aidha amesema Oman imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia uhifadhi na uendelezaji wa majengo ya kihistoria pamoja na utunzaji wa nyaraka.

Amemueleza Balozi huyo kuwa kwa mujibu wa kumbukumbu za kihistoria, Zanzibar na Oman zilikuwa nchi moja, na kutaka uhusiano huo wa kindugu uimarishwe zaidi.

Amesema ni jambo la faraja kuona kuwa Oman imekuwa nchi moja wapo inayozungumza lugha ya Kiswahili nje ya bara la Afrika, hali inayodhihirisha udugu uliopo baina ya Oman na Tanzania.

Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top