Na; Khamis Haji (OMKR)

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameonya kuwa tabia ya baadhi ya watu kuharibu mazingira inasababisha athari kubwa, ikiwemo kupotea eneo kubwa la ardhi ya Zanzibar inayotegemewa kwa shughuli za maendeleo na za kijamii.

Maalim Seif amesema hayo leo wakati alipofanya ziara ya kutembelea maeneo mbali mbali ambayo ardhi yake imeliwa na maji ya bahari katika kisiwa cha Unguja. Akiwa ameambatana na Wakuu wa Mikoa ya Mjini Magharibi, Kaskazini na Kusini Unguja.

Amesema ili hali hiyo iweze kukomeshwa, Viongozi wa Mikoa, Wilaya na taasisi za Serikali zinazohusika na Kilimo na Mazingira zinapaswa kushirikiana kuielimisha jamii kuacha uharibifu wa mazingira, lakini pia kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wote wanaobainika kuharibu wa mazingira.

Akiwa katika ziara hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais alijionea ukuta uliojengwa na mwananchi mmoja katika eneo la ufukwe wa bahari ya Mkokotoni kinyume cha sheria ukiwa juu ya bomba linalopeleka maji katika kisiwa cha Tumbatu.

Kitendo hicho kimeelezwa na Viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na wataalamu wa mazingira kuwa kinaweza kuathiri upatikakanji wa huduma ya maji kwa wakaazi wa kisiwa hicho cha Tumbatu, lakini pia ni uharibifu mkubwa katika ufukwe huo.

Kutokana na hali hiyo, Maalim Seif ameagiza ukuta huo uvunjwe kwa gharama za aliyeujenga, ili kuepusha uwezekano wa wananchi kukosa huduma ya maji, pia kulindwa ufukwe huo na vitendo vya uchimbaji mchanga na ukataji mikoko.

Maeneo mengine aliyoyatembelea ni eneo la Kilimani, Mnazimmoja, Kisakasaka katika Mkoa wa Mjini Magharibi na Pete na Jambiani katika mkoa wa Kusini Unguja.

Maeneo hayo ni miongoni mwa 148 kote Unguja na Pemba ambayo yamekumbwa na athari kubwa kutokana na uvamizi wa maji ya bahari kulikosababishwa na vitendo vya binaadamu kama vile, ukataji mikoko, uchimbaji mchanga, uvuvi haramu, pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Makamu wa Kwanza wa Rais alisema ni lazima sheria za kulinda na kuhifadhi mazingira zilizopo zitumiwe ipasavyo, pia hali ya kuoneana muhali katika utekelezaji wa sheria ipigwe vita, ili kuinusu ardhi ndogo ya Zanzibar isitowekwe kwa kuliwa na maji ya bahari.

Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mazingira Zanzibar, Sheha Mjaja Juma, alieleza kuwa utafiti unahitajika kufanywa katika maeneo hayo na yote yaliyoliwa na maji ya bahari, ili kuweza kuchukuliwa hatua zinazofaa kitaalamu kuyalinda na kuyahifadhi.

Wakati huo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amezitembelea familia pamoja na wenye miradi ya vitegauchumi walioathiriwa na maafa ya upepo mkali ulioambatana na mvua na radi, uliotokea juzi katika eneo la Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Miongoni mwa aliowatembelea ni pamoja na familia ya Naliwe Mbarouk aliyefariki Dunia baada ya kupigwa na radi wakati wa mkasa huo.

Aidha, kufuatia mkasa huo baadhi ya wananchi wameumia na wengine kupata upofu, huku wengine makaazi yao yakiwa yameharibiwa vibaya na upepo huo.

Aidha, alitembelea skuli ya Nungwi ambayo imeathiriwa baada ya kuangukiwa na mti, pamoja na hoteli ya kitalii ya Zulu, ambayo sehemu kubwa ya paa lake imeanguka na baadhi ya sehemu kuharibiwa vibaya.

0 comments:

 
Top