Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amekutana na balozi mpya wa Tanzania nchini Malaysia Dr. Aziz Ponela Mlima, na kumsisitiza kuendeleza diplomasia ya uchumi, ili kukuza uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Amesema nchi za Asia anazokwenda kuiwakilisha Tanzania zikiwemo Malaysia, Indonesia, Philippines, Laos, Brunei na Cambodia, ni miongoni mwa nchi zinazokua kiuchumi katika ukanda huo, na kumtaka kutumia fursa hiyo kuitangaza Zanzibar hasa katika sekta za utalii, uvuvi na viwanda vidogo vidogo.

Akizungumza na balozi huyo nyumbani kwake Mbweni, Maalim Seif amesema mabalozi wana nafasi kubwa ya kutangaza fursa za kiuchumi na uwekezaji Tanzania, na kutaka kuwashajiisha wawekezaji wa nchi hizo kuja kuwekeza Zanzibar.

Akizungumzia kuhusu sekta ya Utalii, Maalim Seif amesema ukanda huo wa nchi za Asia umekuwa ukitoa watalii wengi kwenda nchi za kigeni, lakini bado Tanzania haijaweza kuitumia kikamilifu fursa ya kujitangaza kwa nchi hizo.

Amesema wakati umefika kwa mabalozi kuweka wazi mikakati ya Tanzania katika kukuza uchumi wake, ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa za kiuchumi, biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake balozi huyo wa Tanzania nchini Malaysia Dr. Aziz Mlima, ameahidi kutumia fursa hiyo kuitangaza Tanzania ili iweze kukuza uchumi na uhusiano wake na nchi hizo.

Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top