Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameiagiza Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar kukubaliana na mtu aliyepewa eneo kinaloingia maji ya chumvi lililopo Kilimani, ili liweze kurejeshwa serikalini.

Amesema eneo hilo lililokuwa likitumika kwa shughuli za kilimo, pia lipo karibu na makaazi ya watu pamoja na ofisi za serikali ikiwemo Tume ya Uchaguzi Zanzibar, na kwamba iwapo litaachiwa linaweza kuleta athari kubwa.

Maalim Seif ametoa agizo hilo ikiwa ni siku mbili tu tangu afanye ziara maalum ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyovamiwa na maji ya chumvi katika kisiwa cha Unguja likiwemo eneo hilo la Kilimani.

Akitoa agizo hilo mbele ya Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ramadhan Abdallah Shaaban walipokutana katika eneo hilo, Maalim Seif amesema ofisi yake kupitia Idara ya Mazingira, tayari imeliainisha eneo hilo kuweza kulifanyia utaratibu wa kuzuia maji hayo, lakini haiwezi kufanya hivyo likiwa bado linamilikiwa na mtu binafsi.

Nae Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdallah Shaaban, ameahidi kulifanyia kazi suala hilo kupitia taratibu za kisheria kwa kuangalia umiliki wa mtu aliyepewa eneo hilo.

Amebainisha kuwa iwapo mtu huyo amemilikishwa eneo hilo kisheria, serikali itafanya utaratibu wa kumpatia eneo jengine, ili kuwezesha eneo hilo kurejeshwa serikali haraka iwezekanavyo.

Mapema akitoa ufafanuzi juu ya namna ya kuzuia maji ya chumvi kuingia katika eneo hilo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Islam Seif amesema, mpango huo ulikuwepo muda mrefu lakini walishindwa kuchukuwa hatua kutokana na utata uliokuwepo.

Amefahamisha kuwa iwapo eneo hilo litarejeshwa serikalini, wataendeleza utaratibu walioupanga kwa lengo ya kulidhibiti eneo hilo lisiingie maji ya chumvi na kuweza kutumika kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Amebainisha kuwa njia muafaka zinazoweza kutumika kudhibiti maji hayo ni pamoja na kujenga tuta la kitaalamu, pamoja kuimarisha upandaji wa mikoko.

Jumla ya maeneo 148 tayari yameshabainishwa kuingia maji ya chumvi Unguja na Pemba, huku Kisiwa cha Pemba kikiwa na maeneo mengi zaidi yapatayo 123.

0 comments:

 
Top