Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Sharif Hamad, amesema serikali imepata moyo kuona taasisi, mashirika na wananchi jinsi walivyojitokeza katika maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kujitokeza kwao kwa wingi kunaashiria jinsi wananchi walivyohamasika kuonyesha na kutangaza huduma zao kwa wengine, kwa lengo la kuzitambulisha na kutafuta soko ndani na nje ya nchi.

Mhe. Maalim Seif ameeleza hayo baada ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi yaliyoko Beit- el- Raas, mjini Zanzibar.

Amesema wananchi wameonesha kuyapenda maonyesho hayo ya bidhaa na huduma, na kwamba ni vyema yakaandaliwa kila baada ya muda, bila ya kusubiri miaka 50 mengine.

Maonyesho hayo ya kwanza ya aina yake kufanyika Zanzibar, yamekuwa kivutio kikubwa kwa wenyeji na wageni, yanazishirikisha taasisi mbali mbali zikiwemo taasisi binafsi, mashirika ya umma na wajasiriamali.

Katika ziara hiyo Mhe. Maalim Seif ametembelea mabanda ya maonyesho kwa taasisi tofauti zikiwemo Jumuiya ya Wafanyabiashara, Chuo Cha usimamizi wa fedha, mafunzo ya amali, polisi na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top