Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Moh'd Sheni leo tarehe 2 Januari  2014 anatarajiwa kuyafungua rasmi maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Maonyesho hayo ya siku Nne yanayoshirikisha zaidi ya Taasisi 122 za Serikali pamoja na Zile Binafsi yatafanyika katika uwanja wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Tanzibar { SUZA } uliopo Beit El Ras nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikagua matayarisho ya mwisho ya maandalizi ya maonyesho hayo.

Balozi Seif alipata wasaa wa kuangalia mabanda ya Taasisi hizo ambazo 60 ni za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 49 Taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na taasisi 13 za binafsi.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Maadhimisho ya Kitaifa alionyesha kuridhika kwake na maandalizi ya mwisho ya maonyesho hayo kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na watendaji wa taasisi husika.

Hata hivyo baadhi ya Taasisi za Serikali na hata zile za binafsi zinaonekana kuendelea na matayarisho hayo katika mwendo wa kusua sua.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimalizia ziara yake kwa kuangalia banda la kitengo cha huduma za macho lilioko chini ya Wizara ya Afya ambapo watendaji wa kitengo hicho walimueleza Balozi Seif kwamba huduma za upimaji wa macho zitatolewa muda wote katika siku nne za Maonyesho hayo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top