Uimarishaji wa Sekta ya Viwanda vidogo vidogo kwa kutumia mali ghafi na biadhaa za kilimo zinazozalishwa na wakulima pamoja na wajasiri amali mbali mbali ndio njia pekee itakayoisaidia Serikali na Wananchi katika mpango wa kupunguza   wimbi kubwa la vijana wasio na ajira hapa Nchini.

Mpango huo unaweza kufanikiwa vyema na kuendelea kuwa wa kudumu endapo utekelezaji wake utapata nguvu za kuungwa mkono kati ya Serikali Kuu kwa kushirikiana na Mashirika, Taasisi pamoja na Mataifa washirika wa Maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mdogo wa India aliyepo hapa Zanzibar Bwana Pawan Kumar hapo kwenye Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif aliiomba Serikali ya India kupitia Balozi wake huyo mdogo hapa Zanzibar ambae anakaribia kumaliza muda wake wa kazi za Kidiplomasia hapa Zanzibar kuendelea kuunga mkono sekta ya Kilimo kwa kusaidia mpango huo wa kuimarisha Sekta ya viwanda vidogo vidogo kwa lengo la kupanua wigo wa ajira.

Alisema Visiwa vya Zanzibar vimekuwa vikizalisha mazao mbali mbali ya kilimo ambayo yakitumiwa vyema kwenye viwanda vitakavyoanzishwa vya usindikaji yanaweza kusaidia kustawisha maisha ya wazalishaji hao pamoja na kuongeza mapato ya Taifa.

“ Yapo mazao mengi yanayozalishwa na Wakulima pamoja na wajasiri amali wetu katika maeneo mbali mbali ya kilimo nchini ambayo yanauwezo wa kusindikwa kupitia mfumo wa viwanda vidogo vidogo endapo vitaanzishwa “. Alifafanua Balozi Seif.

Akizungumzia sekta ya Afya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza India kwa jitihada zake za kusaidia huduma za Afya kwa Wananchi mbali mbali wa Zanzibar wanaopelekwa kupatia huduma hiyo Nchini India.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Zanzibar imekuwa ikipeleka wananchi wake wengi wenye matatizo ya kiafya nchini utaratibu ambao unaendelea kuleta faraja kwa Serikali pamoja na familia za wagonjwa wanaopata fursa hiyo.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Serikali ya India kupitia Sekta na Taasisi zake za Afya Nchini humo kufikiria kufungua Tawi la moja kati ya Hosptali zake Maarufu hapa Tanzania ikiwa ni moja na kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.

Alifahamisha pia kwamba ushauri huo endapo utachukuliwa hatua za haraka unaweza kusaidia kuipunguzia gharama Serikali na hata baadhi ya wananchi wanaopeleka wagonjwa wao kupatia huduma za uchunguzi na matibabu ya kiafya moja kwa moja Nchini India.

Kuhusu Sekta ya Elimu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya India kwa mchango wake mkubwa inaotowa wa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na Mrefu wanafunzi na watumishi wa umma hapa Zanzibar.

Balozi Seif alieleza kwamba Zanzibar hivi sasa imefanikiwa kuwa na wataalamu wa fani tofauti waliobahatika kupata elimu ya Juu Nchini India na kumuomba Balozi Pawan kuendelea kusimamia mpango huo ili kupata ufanisi zaidi katika uimarishaji wa sekta za Umma Kitaalamu.

“ Hili suala la mafunzo ya watumishi wetu wakiwemo pia Viongozi waandamizi wa Serikali na Mabaraza ya Kutunga Sheria bado lina umuhimu wake hasa ikizingatiwa mabadiliko ya kasi ya dunia ya Teknolojia yaliopo Ulimwenguni hivi sasa “. Alieleza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na mipango ya kuwapatia mafunzo ya kazi Wajumbe wa Kamati za Baraza lake la Wawakilishi yatakayowapa nguvu imara za kuimarisha utendaji wao.

Naye Balozi Mdogo wa India hapa Zanzibar Bwana Pawan Kumar alisema India iko tayari kuendelea kuunga mkono harakati za kiuchumi za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili kupiga hatua kubwa zaidi za maendeleo.

Balozi Pawan Kumar aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutayarisha maombi maalum ya Wajumbe wa Kamati za Baraza la Wawakilishi na kuyapeleka Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar kwa ajili ya kuwasilishwa Ofisi ya Ubalozi huo kwa hatua za utekelezaji.

Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Viongozi na watendaji wake kwa kushirikiana vyema na Ofisi yake ushirikiano uliomuwezesha kutekeleza vizuri majukumu yake ya Kidiplomasia aliyopangiwa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top