Rais wa Jamuhuri ya Visiwa vya Comoro Mheshimiwa Dr. Ikililou Dhoinine amewasili Zanzibar leo jioni kwa ajili ya kuhudhuria maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika katika uwanja wa amani Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, viongozi wa kiserikali, siasa pamoja na wageni waalika kutoka baadhi ya nchi za kiafrika na zile rafiki.

Kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Mheshimiwa Dr. Ikililou alipokewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif Ali Iddi.

Balozi Seif pia aliambatana na Baadhi ya Mawaziri, makamanda wa Vikosi vya aUlinzi na usalama Nchini pamoja na Wanajumiya ya Wakfi ya Wangazia hapa Zanzibar wakiongozwa Rais wao Profesa Saleh Idriss Ahmed.

Mara baada ya kuwasi Rais huyo wa Jamuhuri ya Comoro na mwenyeji wake Balozi Seif waliangaliwa kikundi cha ngoma za asili kilichotayarishwa rasmi kwa ajili yake.

Jamuhuri ya Comoro imekuwa na uhusian wa muda mrefu na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla hasa kutokana na wananchi wake kuingiliana kidamu jambo ambalo linafanya watu wa pande hizo mbili wawe kama ndugu wa familia moja.

Mheshimiwa Dr. Ikililou Dhoinine anatarajiwa kurejea nyumbani Comoro kesho jioni mara baada ya sherehe za maadhimisho hayo ya miaka 50 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top