Jeshi la Polisi Nchini katika kuhakikisha linaendelea kutekeleza vyema majukumu yake limekumbushwa kuchukuwa hatua za haraka za kudhibiti ishara ya vitendo vya uvunjifu wa amani mara tu linapoanza kuona dalili za muelekeo wa kuchezewa kwa amani ya Nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania IGP Ernest Mangu aliyefika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo mwishoni mwa mwaka uliopita.

Balozi Seif alimueleza IGP Ernest Mangu aliyefuatana na Naibu wake Abdulrahman Omar Juma pamoja na Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame kwamba uchochezi ni jambo la hatari na kwa mujibu wa sheria na taratibu za Nchi linatambulika kuwa ni kosa la jinai ambalo anapaswa muhusika kuchukuliwa hatua za kisheria anapobainika kulifanya kosa hilo.

Alifahamisha kwamba Serikali wakati wote isingependa kuona wananchi wake wanashindwa kuendelea na harakati zao za kimaisha kwa sababu ya watu wachache wenye tabia ya kuchochea uasi unaozaa vurugu zisizo na msingi wowote ule.

Alisema kutokana na mabadiliko ya teknolojia ambayo pia hutumiwa vibaya na wajanja wachache katika kufanya vitendo viovu askari wa jeshi hilo wanapaswa kuwa makini katika kufuatilia vitendo vya baadhi ya watu wanaotiliwa mashaka ndani ya Jamii.

Balozi Seif alifahamisha kwamba hatua hiyo itafanikiwa vyema iwapo makamanda wa jeshi hilo watapanga mikakati imara itakayosaidia kuimarisha zaidi ulinzi kwenye maeneo yenye muelekeo wa kuibuka kwa vitendo hivyo.

“ Serikali isingependa kuona wananchi wanashindwa kuendelea na harakati zao za kimaisha kwa sababu tu ya watu wachache wanaochangia kushawishi vikundi vya kihuni kufanya vurugu katika maeneo yao “. Alisema Balozi Seif.

Akimpongeza Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Kamanda Ernest Mangu kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kulipa ushirikiano zaidi Jeshi hilo katika kuona linatekeleza vyema majukumu lililopangiwa na Taifa.

Mapema Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Ernest Mangu alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Jeshi la Polisi Nchini daima litaendelea kulinda usalama wa raia na mali zao.

IGP Mangu alifahamisha kwamba ulinzi huo utafanikiwa zaidi endapo ushirikiano wa pamoja na wa karibu utakuwepo kati ya jeshi hilo, Wananchi pamoja na viongozi wote, wa Serikali na Kisiasa.

Katika uimarishaji wa jeshi hilo kiutendaji Kamanda Ernest Mangu alieleza kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imekubali kulidhamini jeshi hilo kwa kulipatia magari ili kupunguza changamoto zinazolikabili jeshi hilo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Ndugu Johari Masoud Sururu aliyefika Ofisini kwake Baraza la wawakikilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa rasmi kushika wadhifa huo Tarehe 24 Novemba Mwaka 2013.

Katika mazungumzo yao Mkurugenzi huyo wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Nd. Johari Masoud Sururu alisema Idara hiyo katika kwenda na wakati inatarajia kuanza kutumia Mtambo mpya wa Kisasa wa huduma za wasafiri katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.

Mkurugenzi Sururu alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua hiyo imekuja ili kujaribu kupunguza au kuondosha kabisa msongamano uliopo wa wasafiri kwenye uwanja huo.

Alifahamisha kwamba mpango huo pia utakwenda sambamba na Taasisi hiyo kuanza ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wake ili kukabiliana na tatizo la makazi ambalo huleta usumbufu kwa watendaji hao.

Akimpongeza Mkurugenzi huyo wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Ndugu Johari Masoud Sururu kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi huo wa Idara ya Uhamiaji kuandaa utaratibu makini utakaosaidia kudhibiti uvujaji wa mapato yanayotokana na uingiaji wa wageni kwenye viwanja vya ndege na bandarini hapa Nchini.

Balozi Seif alisema bado wapo baadhi ya watendaji wa Taasisi hiyo wanaoonekana kutumia ujanja wakati wanaposimamia ukusanyaji wa mapato yatokanayo na wageni wanaoingia Nchini.

Akizungumzia suala la usalama wa nchi linalokwenda sambamba na wageni wanaiongia Nchini Balozi Seif aliitahadharisha Taasisi hiyo ya Uhamiaji kuwa makini na uingiaji wa wageni kiholela.

Alisema wakati umefika kwa jeshi hilo kujiandaa kudhibiti watu au vikundi vya watu vyenye ishara ya kutaka kuingia nchini kwa kujihusisha na vitendo vyovyote vyenye muelekeo wa kuleta hujuma nchini.

“ Tumeshuhudia majirani zetu waliotuzunguuka ambao wamepatwa na misuko suko ya hujuma za uvunjifu wa amani, maafa na hata uharibifu wa mali za raia kutokana na kudharau baadhi ya vikundi vilivyokuwa vikijipenyeza ndani ya nchi hizo “. Alitahadharisha Balozi Seif.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top