Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi alisema katika kuunga mkono nguvu za Wananchi za kujiletea maendeleo katika maeneo yao mbali mbali Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusaidia miradi ya kiuchumi na kiustawi wa Jamii ili kuona juhudi za Wananchi hao zinafikia kwenye maendeleo yaliyokusudiwa.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Unguja Ukuu Kaepwani mara baada ya kuweja Jiwe la Msingi la Jengo Jipya la Soko ya Kuuzia Samaki liliopo pembezoni mwa Bahari ya Kijiji hicho ambalo linajengwa kwa nguvu za Viongozi na Wananchi wenyewe.

Balozi Seif Ali Iddi lisema Serikali itajitahidi kuona jengo hilo linamalizika kwa wakati na akawataka wananchi hao wamalizie ujenzi wa vibaraza vya ndani ya jengo hilo ambapo yeye binafsi aliahidi kuchangia shilingi Laki 500,000/- kutekelezwa kazi hiyo ili kuipakasi Serikali Kuu imalizie masuala yaliyobakia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza wananchi hao kwamba Serikali pia itajitahidi kuwapatia boti maalum kwa ajili ya uokozi wa wavuvi pale inapotokea ajali wakati wakiwa katika shughuli zao za uvuvi.

Aliwapongeza Wananchi hao kwa uwamuzi wao wa kujenga jengo la kudumu la kuuzia samaki na kusisitiza kwamba maeneo ya uvuvi ni lazima wakati wote yawe katika mazingira bora.

Akisoma risala ya Wananchi wa Jimbo la Koani Mwalimu Makame Haji Steni alisema ujenzi wa soko hilo umekuja kufuatia tatizo kubwa la mauzo ya samaki lililokuwa likiwakumba wavuvi wa maeneo hayo.

Mwalimu Makame alisema wavuvi hao walikuwa wakilazimika kuuza samaki wao masoko na Mjini kitendo ambacho kilikuwa kikiwakosesha mapato makubwa na kujikuta wakipata hasara.

Ujenzi wa soko hilo ulioanza mwaka 2013 umefikia gharama ya shilingi Milioni 11,000,000/- zilizotokana na mchango wa Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Koani kwa ushirikiano wa nguvu za Wananchi wenyewe.

Soko hilo la kisasa litakapokamilika linatarajiwa kuhudumia wavuvi wa Vijiji vya N’gambwa, Uzi na Unguja Ukuu yenyewe.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top