Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefikia uamuzi wa Mashamba yote ya Serikali yaliyokuwa chini ya usimamizi na uangalizi wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kuanzia sasa yatasimamiwa na Wizara ya Kilimo na Mali asili Zanzibar.

Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kuzingatia kwa kina kwamba Wizara ya Kilimo na Maliasili ndio yenye dhamana ya kusimamia uhuishaji wa miti hasa mikarafuu na minazi ambayo ndio inayoonekana kusheheni zaidi katika mashamba hayo.

Hati za makabidhiano ya usimamizi wa mashamba hayo ya Serikali zilifanyika katika ukumbi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania { Tasaf } wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar uliopo Chake chake Kisiwani Pemba na kushirikisha pia watendaji wa Wizara zote mbili.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Nd. Ali Khalil Mirza alimkabidhi hati hizo Katibu Mkuu mwenzake wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Nd. Afan Othman Maalim tukio ambalo lilishuhudiwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Akikabidhi hati hizo Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Nd. Ali Khalil Mirza alisema Wizara hiyo ilikuwa ikidhibiti mashamba 111 ya Eka Tatu Tatu Unguja na Pemba kuanzia mwaka 1989 ambayo wananchi waliokuwa wakiyatumia kwa shughuli zao za Kilimo kwa sasa wamefariki Dunia.

Nd. Mirza alisema hati hizo zilizomo kwenye madaftari Manne zinaonyesha rikodi zote za uwepo wa mashamba 8,215 ya eka tatu tatu Zanzibar ambazo kwa mujibu wa sera za mabadiliko ya ardhi zilikuwa chini ya iliyokuwa Kamisheni ya Ardhi na Mazin gira tokea mwaka 1989.

Akipokea Madaftari hayo yenye hati za kumbu kumbu za mashamba hayo ya Serikali Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali asili Nd. Afan Othman Maalim aliwaomba watendaji wa Wizara ya Ardhi kuendelea kutoa ushirikiano wa utambuzi wa Mashamba hayo kwa lengo la kulinda Mali za Serikali.

Nd. Afan alifahamisha kwamba kutokana na umuhimu uliojitokeza hivi sasa wa matumizi makubwa ya mashamba unaotokana na mabadiliko ya Dunia bila shaka zinaweza kujitokeza hitilafu na changamoto zitakazohitaji kutatuliwa kwa pamoja kati ya taasisi hizo.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Baraza lake la Mapinduzi iliamua kuunda kamati Maalum kujaribu kufuatilia kasoro zilizomo za matumizi mabaya ndani ya mashamba yote ya Serikali.

Balozi Seif alifahamisha kwamba ripoti ya Kamati hiyo ilithibitisha kwamba mengi ya mashamba ya Serikali hasa yale yaliyokuwa yalisimamiwa na Wizara ya Ardhi, Makazi, maji na Nishati yalikosa usimamizi mzuri.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitolea mfano Mashamba mengi ya mikarafuu hasa Kisiwani Pemba kwa kipindi kirefu yalikosa huduma inayostahili na kusababisha upungufu wa uzalishaji wa zao la Karafuu.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa { UN } hapa Tanzania Bwana Alberic Kacou hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Alberic ambae anamaliza utumishi wake Nchini Tanzania na kujiandaa kurejea Makao Makuu ya Umoja huo Mjini New York Nchini Marekani aliushukuru uhusiano wa karibu uliopo kati ya Tanzania na Umoja.

Alisema uhusiano huo ulimwezesha kutekeleza majukumu yake kwa kiwango kinachokubalika na kuwa kiungo muhimu cha utendaji kati ya Taasisi za Umoja wa Mataifa na Serikali zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tnaznia na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mratibu Mkaazi huyo wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania aliahidi kwamba Umoja huo kupitia Taasisi zake utaendelea kuunga mkono Serikali zote mbili Nchini Tanzania katika kuwapatia maendeleo ya Kiuchumi na ustawi wa jamii wananchi wake.

“ Zipo program kadhaa za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa katika sekta za afya, Kilimo, Mazingira na mawasiliano ambazo zimeanza kutekelezwa tokea mwaka 2011 hadi mwaka 2013 “. Alifafanua Bwana Alberic Kacou.

Akizungumzia suala la siasa Mratibu Mkaazi huyo wa Umoja wa Matifa Nchini Tanzania Bwana Alberic Kacou aliiwapongeza Wananchi wa Zanzibar kwa uamuzi wao wa kuendesha Serikali katika Mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Alisema hatua hiyo ya kupigiwa mfano Duniani ambayo inafaa kuigwa na baadhi ya Mataifa yenye mizozo ya kisiasa hasa Barani Afrika imesaidia kupunguza joto la kisiasa ndani ya visiwa vya Zanzibar katika kipindi kirefu.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi na Mashirika yake mbali kwa juhudi zake za kusaidia maendeleo ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii hapa Nchini.

Balozi Seif alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla hivi sasa zimepiga hatua kubwa ya maendeo jambo ambalo limepunguza kasi ya ukali za maisha miongoni mwa wananchi wake.

Hata hivyo Balozi Seif alisema tatizo kubwa linalikabili Taifa kwa wakati huu ni tatizo la ongezeko la matumizi ya Dawa za kulevya linalooonekana kuwaathiri zaidi Vijana.

Alieleza kwamba wapo baadhi ya watu na taasisi zilizojitolea kuweka nyumba maaluma za kurekebisha tabia za kuachana na dawa za kulevya hatua ambazo zinahitaji kuungwa mkono na taasisi na mashirika ya kitaifa na kimataifa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top