Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amezipongeza Taasisi na Mashirika ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na zile binafsi kwa ushiriki wao katika maonyesho ya siku Nne kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pongezi hizo alizitoa mwishoni mwa maonyesho hayo alipotembelea baadhi ya Mabanda hapo katika uwanja wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } uliopo Beit El Ras Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Taifa ameelezea kuridhikwa kwake na hatua iliyofikiwa na taasisi hizo jambo ambalo limeleta faraja kwa Serikali pamoja na Taasisi hizo.

Alisema maonyesho ni moja ya sehemu ya kujifunza, kubadilishana mawazo pamoja na kupata wigo wa kutafuta soko kwa bidhaa na vifaa vinavyotengenezwa na baadhi ya Taasisi husika.

Alisema wakati Serikali inajipanga vyema kuhakikisha suala la Maonyesho linaendelea kuwa la kudumu akazisisitiza Taasisi na Mashirika hayo ya Serikali nay ale ya Binafsi kuongeza juhudi zaidi ili kuona utaratibu wa kuwepo maonyesho unanufaisha wananchi walio wengi.

“ Umefika wakati sisi kama sehemu ya Dunia tunalazimika kuwa makini katika kuyatumia maonyesho katika kujitangaza kitaalamu kibiashara ulimwenguni “. Alifafanua Balozi Seif.

Baadhi ya wawakilishi wa Taasisi zilizoweka mabanda yao kwenye maonyesho hayo walimueleza Balozi Seif kwamba Serikali zote mbili ni vyema zikaendeleza mipango ya kuimarisha maeneo ya maonyesho ambayo yanaonekana kutoa fursa nzuri hasa kwa wajasiria amali kuweza kujitangaza.

Mwakilishi wa Zana, Dawa na Bidhaa za Kilimo wa Jumuiya ya Kilimo ya Ilala { Farmer Centre } Bibi Zahra Karim Zam alisema Taasisi yao imeshajiandaa kufungua tawi la hapa Zanzibar ili kuwarahisishia upatikanaji wa Vifaa vya Kilimo Wakulima wa Zanzibar.

Bibi Zahra alifahamisha kwamba wakulima wengi wamekuwa wakiendesha shughuli zao za Kilimo bila ya utaalamu wa kutosha jambo ambalo linawakosesha mapato mazuri.

Alieleza kwamba Taasisi, Jumuiya na hata wataalamu waliopo hivi sasa Nchini Tanzania Bara na Zanzibar endapo watatumiwa vyema sekta ya kilimo inaweza kuleta mabadiliko ya haraka.

Maonyesho hayo ya siku Nne yalishirikisha jumla ya Taasisi 124 kati ya hizo 60 ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Taasisi 49 za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na 13 kutoka Taasisi binafsi bara na Zanzibar.



Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top