Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel imejipanga kuongeza uzalishaji kupitia mfumo wa kisasa wa mawasiliano utakaokwenda sambamba na kutanua kwa ongezeko la ajira litakalosaidia zaidi vijana wazalendo hapa Nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Mtandao wa Mawasiliano kupitia mfumo wa satalaiti la Etisalat linaloendesha Kampuni ya Zantel Bwana Pralap Ghose wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Pralap alisema uongozi wa Kampuni ya Zantel unaendelea kufanya mawasiliano na Taasisi zinazohusika na ajira hapa Nchini ili kuona mpango wao huo unafanikiwa kwa kiasi kikubwa ukiwa na lengo la kuisaidia Serikali kupunguza ukali wa maisha miongoni mwa wananchi wake.

Mwakilishi huyo wa Etisalat alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba licha ya Kampuni hiyo kutanuka zaidi kibiashara ndani ya kipindi cha miezi sita lakini Uongozi wake umekusaidia kuongeza uzalishaji utakaosaidia pia kunyanyua uchumi wa Taifa.

Alifahamisha kwamba mfumo wa usafirishaji wa fedha unaotumiwa na wateja wa Kampuni hiyo wa ezypesa mbali ya kutoa ajira kwa vijana walio wengi nchini lakini pia unatoa unafuu kwa wateja wao kutumia muda wao kwa mambo mengine badala ya kushughulikia taratibu za kutuma fedha kwa jamaa zao.

Hata hivyo Bwana Pralap alisema zipo baadhi ya changamoto zinazokwaza shirika hilo katika kuelekea kwenye ufanisi zaidi akatolea mfano wa tatizo la kodi inayolipa Kampuni hiyo kwa Taasisi mbili za ukusanyaji wa mapato hapa Nchini za Mamaka ya Mapato Tanzania { TRA } na Bodi ya Mapato Zanzibar { ZRB }.

“ Sisi huduma tunazotoa zimelenga kuwahusisha wananchi wote Tanzania Bara na Zanzibar. Lakini tunapambana na kikwazo wakati tunapolipa kodi, tunajikuta tukilazimika kulipa kodi kwa Bodi na Mapato Zanzibar { ZRB } na Mamlaka ya Mapato Tanzania { TRA }. Ukweli inafikia wakati tunakuwa njia panda “. Alifafanua Bwana Pralap.

Mwakilishi huyo wa Shirika la Etisalat alifahamisha kwamba Uongozi wa Taasisi hiyo kupitia Kampuni ya Zantel unaendelea na mazungumzo na baadhi ya Taasisi hapa nchini ili zishirikiane katika kutoa huduma mbali mbali za fedha kupitia mtandao wa Kampuni hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya Zantel Zanzibar Mohamed Mussa akizungumzia ushiriki wa Kampuni hiyo katika maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar alieleza kwamba Taasisi hiyo inakusudia kuweka mabango maalum yatakayosaidia kuonyesha sherehe hizo moja kwa moja kutoka uwanja wa amani.

Mohamed Muusa alisema kazi hiyo inayotarajiwa kutekelezwa kwa pamoja kati ya kampuni hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar itatoa fursa kwa wananchi wasiopata fursa ya kuhudhuria sherehe hizo kuziona wakati huo huo katika baadhi ya sehemu kwenye manispaa ya Mji wa Zanzibar.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alilipongeza shirika hilo la Etisalat kupitia Kampuni yake ya Zantel kwa hatua iliyofikia ya kutoa huduma za mawasiano kwa wananchi.

Balozi Seif alisema huduma za mawasiliano hivi sasa zimesaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwa Mataifa mbali mbali na hasa kwa jamii katika sehemu tofauti mijini na vijijini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia uongozi wa Shirika hilo la Etisalat kupitia Kampuni yake ya Zantel kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaifuatilia changamoto inayoikabili kampuni hiyo hasa suala la ulipaji wa kodi kwa Taasisi mbili ili kuiondoshea kero Kampuni hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar’

0 comments:

 
Top