Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na jitihada za kuimarisha huduma za viwanja vya ndege viendane na hadhi ya Kimataifa Wananchi wameombwa kuheshimu mipaka ya viwanja hivyo kwa lengo la kujiepusha na kujenga karibu na maeneo ya viwanja hivyo.

Ujenzi huo endapo utaachiliwa uendelee baadaye unaweza kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi hao hasa wakati Serikali inapopata nguvu zaidi za kutaka kuongeza miundo mbinu ya upanuzi wa viwanja hivyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la jengo jipya la Abiria na bara bara ya maegesho ya ndege katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ikiwa ni mfululizo wa maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 50.

Balozi Seif alisema mradi huo mkubwa wa ujenzi wa jengo la abiria na bara bara za kurukia na maegesho ya ndege ambao ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 umelenga kuimarisha uchumi wa Nchi kwa manufaa ya wananchi wote wa Zanzibar.

“ Miradi hii itakapokamilika itapelekea kuimarisha uchumi wa Nchi yetu kwani kiwango cha ndege za kimataifa kitaongezeka mara dufu ikiwemo mizigo pamoja na abiria “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa sekta ya utalii ambayo ndio sekta kuu kwa uchumi wa Zanzibar itaimarika zaidi kufuatia kukamilika kwa mradi huo na kutoa fursa pia kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kuuza bidhaa zao na kupunguza ukali wa maisha kutokana na kuongezeka kwa uingiaji wa wageni hapa nchini.

Alifahamisha kwamba kipindi cha miaka hamsini ya Mapinduzi ya Zanzibar, huduma za viwanja vya ndege zimeimarika nchini na kuongezeka kwa Makampuni mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa yanayotoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo nje ya Tanzania.

Aidha Balozi Seif alieleza kwamba Serikali tayari imeshajipanga kuimarisha miundombinu ya kiwanja cha ndege cha Kisiwani Pemba kwa kukiwekea taa ili kiweze kutoa huduma saa 24.

Alisema ukosefu wa taa kiwanjani hapo ni tatizo kubwa linalopelekea huduma za ndege kukosekana wakati wa usiku jambo ambalo ni hatari hasa wakati inapoweza dharura muhimu ya utumiaji wa ndege wakati wa usiku kisiwani humo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Mamlaka ya uwanja wa ndege kwa kuimarisha huduma pamoja na kuboresha mazingira na kuutaka kuzidisha juhudi na ubunifu ili uwanja huo ulingane na viwanja vyengine vya Kimataifa katika kulinda usalama na usafi wa mazingira yake.

“ Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar tunataka uwe kama wa wenzetu wa Dubai. Kwa nini wao waweze na sisi tusiweze ? Tunayo mifano hai ya viwanja vya wenzetu ambavyo utakuta wafanyakazi wanafanya kazi muda wote. Kila saa ufyagio mkononi, wafanyakazi wetu lazima waige mfano huu “. Alisema Balozi Seif.

Aliwashukuru washirika wa maendeleo hasa Benki ya Exim ya China pamoja na Benki ya Dunia { World Bank } kwa juhudi zao za kuunga mkono harakati za maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Balozi Seif aliwaomba washirika hao wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa kutoa misaada na mikopo yenye masharti nafuu.

Mapema Naibu katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Nd.Talib Abdulla alisema kukamilika kwa mradi huo wa jengo la abiria utaweza kuhudumia abiria wapatao laki 156,000 kwa mwaka wakati eneo la maegesho ya ndege litakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa tatu kwa wakati mmoja.

Nd. Talib alisema mradi wa upanuzi wa maegesho ya ndege hivi sasa umefikia asilimia 55%,wakati upanuzi wa njia za kupitishia ndege umefikia asilimia 98% na njia za kuunganisha ndege uko katika asilimia 80%.

Hata hivyo naibu katibu mkuu huyo wa Miundombinu na Mawasiliano alisema zipo changamoto zilizosababisha kuchelewa kwa mradi huo akizitaja kuwa ni pamoja na ujazazji wa mashimo makubwa pamoja na kuwepo kwa mawe mengi katika eneo hilo la mradi.

Mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria unategemewa kutumia jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 82.6 mkopo kutoka Exim Benki ya China ambapo mchango wa SMZ ukiwa shilingi za Kitanzania Bilionimbili { 2,000,000,000/- } wakati ujenzi wa njia za maegesho ya ndege utagharimu Dola Milioni 75.8 mkopo wa Benki wa Dunia ambapo SMZ itatoa shilingi Bilioni 1.36.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa alipokea mchango wa fedha kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Quality Group ambae pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya soka ya Yanga ya Dar es salaam Bwana Yussuf Manji ili kusaidia kuchangia sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 50.

Bwana Manji ambae alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ushiriki wa Timu yake ya Yanga katika mashindano ya Mapinduzi Cup alikabidhi mchango huo nyumbani kwa Balozi Seif Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema Kampuni yake pamoja na Timu yake imehamasika kutoa mchango huo wa Shilingi Milioni Kumi na Tano { 15,000,000/- } kufuatia umuhimu wa Tanzania kukabiliwa na sherehe hizo kubwa za maadhimisho ya Nusu karne ya mapinduzi ya Zanzibar.

Akipokea mchango huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimpongeza Bwana Yussuf Manji kwa uwamuzi wa Taasisi zake kuona umuhimu wa kusaidia sherehe hizo zilizokabiliwa na masuala mengi kutokana na umuhimu wake kihistoria.

Balozi Seif alimuhakikishia Kiongozi huyo wa Quality Group na Timu ya Soka ya Yanga pamoja na wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano iko katika utaratibu wa kukamilisha maandalizi ya mwisho ya maadhimisho hayo.



Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top