Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuweka kipaumbele katika kuendeleza mpango maalum wa kufanywa utafiti katika maeneo yote ya Kiuchumi, maendeleo na ustawi wa jamii.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa mazungomzo yake na Ujumbe wa Viongozi Wanane kutoka Serikali ya Swisszerland unaoongozwa na Waziri wa Sayansi, Utafiti na Elimu Bwana Mauro Dell Ambrogio aliokutana nao hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema mpango huo utakwenda sambamba na ongezeko la mitaala pamoja na masomo ya utafiti kupitia skuli za Sekondari na vyuo vikuu ili Taifa lifikie daraja ya kujitosheleza kwa wataalamu wa fani hiyo kufikia daraja la Udaktari.

Aliueleza Ujumbe huo wa Serikali ya Swisszerland ambao upo Zanzibar kuhudhuria Kongamano la Utafiti na Ubunifu Zanzibar la kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zimebahatika kuwa na rasilmali nyingi baharini na Ardhini.

Alifahamisha kwamba Rasilmali hizo hadi sasa bado hazijatumika vyema kutokana na ukosefu wa Taaluma ya kina ya utafiti ambazo baadaye zinaweza kusaidia ustawi wa kipato cha Wananchi walio wengi pamoja na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifafanua kwamba zipo baadhi ya tafiti zilizowahi kufanywa na baadhi ya wataalamu wa hapa nchini kwa kushirikiana pia na wale wa kigeni lakini mara nyingi tafiti hizo huishia kuwekwa maofisini bila ya kufanyia kazi zilizokusudiwa.

Mapema Waziri wa Sayansi, Utafiti na Elimu wa Swisszerland Bwana Mauro Dell Ambrogio ameipongeza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutokana na mipango yake ya kutilia mkazo suala la utafiti.

Bwana Mauro alieleza kwamba utafiti popote pale ndio silaha na uti wa mgongo wa harakati za maendeleo katika taasisi zote ziwe za kiserikali, Mashirika ya Umma na hata sekta Binafsi.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi na Utafiti ya chuo Kikuu cha Basel Nchini Swisszerland Bwana Marcel Tanner aliyekuwa miongoni mwa ujumbe huo alisema Taasisi mbali mbali Duniani hivi sasa zimejikita zaidi katika kuona suala la Utafiti linapewa msukumo unaostahiki.

Bwana Tanner alisema kuwa umuhimu wa tafiti hasa katika sekta za Afya na Kilimo ndio chachu inayosaidia kustawisha maendeleo na ustawi wa jamii popote pale Ulimwenguni.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top