Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema skuli binafsi zina mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini.

Mhe. Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika sherehe za mahafali ya kumi na moja ya skuli ya Kiislamu ya Daarul Arqam, iliyoko Kigamboni Dar es Salaam.

Amesema mchango unaotolewa na skuli binafsi unapaswa kuungwa mkono, ili kuhakikisha kuwa sekta ya elimu inapata maendeleo makubwa mijini na vijijini.

Ameipongeza skuli hiyo kwa kuwa na malengo ya kutaka kuiendeleza hadi kufikia Chuo Kikuu, hatua ambayo itasaidia kunyanyua kiwango cha elimu nchini, sambamba na kuwaondoshea usumbufu wanafunzi wa maeneo hayo.

Amefahamisha kuwa katika kuimarisha ubora wa elimu, ni vyema mtaala wa elimu ukaangaliwa upya, ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu itayowasaidia baada ya kuhitimu masomo yao.

Amesema mtaala wa sasa bado haujatoa kipaumbele kwa mafunzo ya amali, na kwamba wakati umefika kufikiria kwa umakini jambo hilo, ili wanafunzi wanaohitimu waweze kujiajiri wenyeye, na kuacha kutegemea ajira kutoka serikalini ambayo haitoweza kuajiri wahitimu wote.

Amewashauri kutilia mkazo masomo ya sayansi na mawasiliano ya habari (ICT), ili kwenda sambamba na mahitaji ya wakati huu wa sayansi na teknolojia, na kuweza kukabiliana na soko la ajira.

Katika hatua nyengine Mhe. Maalim Seif amewakumbusha wahitimu hao kuendeleza maadili mema waliyoyapata skulini hapo, na kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya.

Pia ametumia fursa hiyo kuuasa uongozi wa skuli hiyo kutilia mkazo elimu ya uhifadhi wa mazingira, ili kudhibiti uharibifu wa mazingira ambao umekuwa miongoni mwa changamoto kubwa za dunia.

Aidha amewataka waislamu wenye uwezo kuwekeza katika elimu, ili kuwaendeleza vijana kitaaluma na kuwajengea misingi imara ya maisha yao ya baadae.

Amewashauri wazazi na walezi kuwaondoshea vikwazo watoto wa kike vikiwemo biashara na kuwaozesha waume wakiwa wadogo, ili kuwaandaa vyema kukabiliana na hali ya maisha.

Mapema Maalim Seif aliweka jiwe la msingi katika jengo la Maabara ya skuli hiyo, na kuahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji ili kuendeleza ujenzi huo.

Kwa upande wake Meneja wa Skuli hiyo Bw. Abdul Aziz Shawwal Msami, amempongeza Makamu wa Kwanza wa Rais kwa juhudi anazozichukua katika kusogeza mbele maendeleo ya elimu nchini.

Ameiomba serikali kuangalia namna ya kupunguza kodi katika uendeshaji wa taasisi binafsi za elimu, ili kuziwesha kutimiza malengo waliyojiwekea.

Skuli hiyo ya maandalizi, msingi na sekondari, pamoja na mambo mengine imekuwa ikifundisha lugha za kigeni, Quran, maadili ya kiislamu na michezo.



Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top