Jeshi la Polisi Nchini limetakiwa kuongeza ushirikiano wa karibu zaidi na Ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka ili kuona imani ya wananchi kwa jeshi hilo inaendelea kubakia wakati wote hapa Nchini.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Kamishna Mpya wa Jeshi la Polisi Zanzibar Kamishna Hamdan Omar Makame aliyefika kujitambulisha rasmi hapo katika Ofisi yake iliyopo kwenye jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema wananchi wamekuwa wakilalamikia matatizo yanayojitokeza kwenye kesi mbali mbali zinazowahusu baadhi ya watu ambazo huleta athari ndani ya jamii na baadhi yake hufifia bila ya wahusika kutiwa hatiani kwa madai ya kukosekana kwa ushahidi.

Alisema hali hiyo ikiachiliwa kuendelea ambayo iko chini ya dhamana ya uwajibikaji wa vyombo hivyo viwili inaweza kuleta sura mbaya na matokeo yake itafikia wakati wananchi kujichukulia hatua mikononi mwao.

“ Tumeshuhudia matukio mbali mbali yenye kutia wasi wasi kwa jamii katika maeneo yao vikiwemo vitendo vya mauaji, udhalilishaji, ujambazi na hata hili lililoibuka la watu kumwagiwa tindi kali. Lakini matokeo yake uchunguzi huo hufifia bila ya jibu muwafaka wanalolipata wananchi “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi wa Jeshi hilo kuzidisha mashirikano yake na wananchi pamoja na taasisi zote ili kuona usalama wa raia na mali zao unaendelea kupatikana hapa nchini.

Balozi Seif alimueleza Kamishna huyo mpya wa Polisi Zanzibar kwamba Ofisi yake kwa vile ndiyo inayoratibu masuala yote ya Muungano hapa Zanzibar itakuwa tayari wakati wote kumpa ushirikiano utakaomuwezesha kutekeleza vyema jukumu alilokabidhiwa na Taifa yeye na askari wake.

“ Ofisi yangu ndio iliyopewa jukumu la kuratibu masuala yote yanayohusu mambo ya Muungano kwa hapa Zanzibar. Hivyo nakuhakikishia kwamba mlango wa Ofisi yangu utakuwa wazi wakati wowote unapopata tatizo la kiutendaji usione tabu kunifuata “. Alisisitiza Balozi Seif.

Hata hivyo Balozi Seif alimueleza Kamishna Hamdan Omar Makame kwamba ipo changa moto hasa wakati wa muelekeo wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 jambo ambalo jeshi hilo linapaswa kujipanga mapema katika kuhakikisha amani ya jamii inaendelea kuwepo Nchini.

Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba atatekeleza vyema majukumu aliyokabidhiwa na Taifa katika misingi ya haki na uadilifu.

Kamishna Hamdan aliyepewa jukumu la kusimamia Kamisheni ya Polisi Zanzibar alieleza kwamba anachokitarajia katika muda wote wa utumishi wake ni kupata ushirikiano wa karibu kutoka pande zote mbili zile za viongozi pamoja na raia wa kawaida.

Kamanda Hamdan Omar Makame alipandishwa cheo na Jemedari Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete na kuwa Kamishna wa Polisi Tarehe 3/12/2013 na baadaye kuteuliwa kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.

Nafasi hiyo ya Ukamishna Zanzibar ilikuwa ikishikiliwa na Bwana Mussa Ali Mussa ambaye kwa sasa ameteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Kamishna wa Polisi Jamii.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top