Mheshimiwa Rashid Seif Suleiman, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano,
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Mheshimiwa Katibu Mkuu, Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini/Magharibi, Unguja,
Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi - Zanzibar.
Waheshimiwa Viongozi mbali mbali wa Vyama vya Siasa na Serikali,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Asaalam Aleykum,

Ndugu Wananchi,
Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa wazima wa afya na kutuwezesha kukusanyika hapa kwa lengo la kuadhimisha sherehe za miaka hamsini (50) ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal II) na pamoja na njia na maegesho ya ndege (Taxway and Apron).

Pia napenda kuushukuru Uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa heshima kubwa walionipa kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika shughuli hii muhimu ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari, 1964.

Ndugu Wananchi,

Ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal II) pamoja na njia na maegesho ya ndege (taxway na apron) ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume ili kiweze kufikia hadhi ya juu ya Kimataifa katika kutoa huduma kwa abiria na ndege zinazoingia na kutoka kwa lengo la kuimarisha uchumi wa nchi yetu kwa manufaa ya wananchi wote wa Zanzibar. 
 
 Ujenzi wa jengo jipya la abiria pamoja na ujenzi wa njia na maegesho ya ndege ni miongoni mwa hatua ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010- 2015 ambazo tulikuwa tukizinadi kwenu wakati wa kipindi cha kuomba ridhaa kutoka kwenu ya kuiongoza nchi hii, miongoni mwa ahadi ni kwamba tutaimarisha huduma za kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume ili kiweze kufikia hadhi ya Kimataifa na leo hii tunathibitisha utekelezaji wa ahadi zetu kwa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal II) ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 1,600,000 kwa mwaka na huduma zote zinazositahiki kwa abiria pamoja na njia na maegesho ya ndege ambayo itakuwa na uwezo wa kukaa ndege aina ya CODE E. 3 na CODE C. 5 – yaani ndege za aina ya Boeing 737 na 777.

Ndugu Wananchi,

Nimeelezwa kwamba mradi wa ujenzi wa Terminal (II) umeanza rasmi tarehe 10 Januari, 2011 na unategemewa kukamilika mwezi wa nne, 2015. Aidha, ujenzi wa jengo jipya la abiria linalojengwa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd. kutoka nchini China na chini ya uangalizi wa Kampuni ya ADPI kutoka Ufaransa, unategemewa kutumia jumla ya Dola 82.6 Million ambazo ni mkopo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo (Exim Bank) kutoka China. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachangia jumla ya T.Shs: 2,000,000,000.

Kwa upande wa ujenzi wa njia na maegesho ya ndege, ujenzi wake unatekelezwa na Kampuni ya M/S SOGEA – SATOM na ulianza rasmi tarehe 20 Agosti, 2012 na unategemewa kukamilika tarehe 15 Mei, 2014 chini ya usimamizi wa Kampuni ya JBG Gauff Ingineure GmbH & Co. KG in Association with M/s NIMETA Consulting (T) kutoka Tanzania na unategemewa kutumia jumla ya T.Shs: 75.8 Bilioni hadi kukamilika kwake ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachangia T.Shs. 1.36 Bilioni katika mradi huo.

Miradi hii itakapokamilika itapelekea kuimarisha uchumi wa nchi yetu kwani kutakuwa na kiwango kikubwa cha ndege za Kimataifa zitakazoingia hapa nchini ikiwemo za mizigo na abiria. Aidha, sekta ya utalii ambayo ndio sekta kuu kwa uchumi wa Zanzibar itaimarika na kupelekea kukua kwa uchumi wa Taifa letu. Lengo la Serikali katika sekta ya utalii ni kupokea zaidi ya watalii 250,000 ifikapo mwaka 2015. Kwa hivyo, mradi huu utasaidia sana kufikia lengo hilo.

Vile vile, wafanyabiashara wadogo wadogo nao, biashara zao zitaimarika na kupata kipato ambacho kitawapunguzia ukali wa maisha. Ni matumaini yangu kuwa jengo hili litakapokamilika litatoa nafasi nyingi za ajira ambapo wajasiriamali wataitumia nafasi hii kuimarisha shughuli zao za kibiashara ili kupunguza umasikini wa kipato na hatimae kuweza kujipatia mahitaji yao ya msingi.

Ndugu Wananchi,

Serikali ya awamu ya saba kwa muda mfupi imeweza kutekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya Uchaguzi, licha ya hali ngumu ya uchumi inayoikabili nchi yetu. 
 
  Naomba nichukuwe fursa hii kueleza kwa muhtasari, juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za viwanja vya ndege, Zanzibar. Serikali ilichukuwa hatua ya kuanzisha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa lengo la kuboresha huduma za viwanja vya ndege ili ziendane na hadhi ya Kimataifa.  
 
Aidha, Serikali tayari imeshajipanga kuimarisha miundombinu ya Kiwanja cha ndege cha Pemba kwa kuweka taa katika kiwanja hicho ili kiweze kutoa huduma wakati wa usiku, kwa sasa hivi kiwanja hicho kinatoa huduma wakati wa mchana tu kiasi ambacho ni tatizo kubwa kwani ikitokea dharura ya kwenda au kuondoka Pemba wakati wa usiku au imetokea dharura ya aina yoyote ile, huwa ni tatizo kwa sababu ya ukosefu wa taa za kuongozea ndege wakati wa kuruka na kutua katika kiwanja cha ndege cha Pemba. Serikali inajitahidi kwa kila njia ili kuhakikisha kuwa kiwanja hicho nacho kinakidhi haja.

Ndugu Wananchi,
Juhudi hizi zinazochukuliwa na Serikali zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na umoja na mshikamano uliopo hapa Zanzibar katika kutekeleza majukumu yetu. Ni imani yangu kuwa juhudi hizi tutazidumisha na kuziendeleza kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi yetu. Sote tunafahamu kuimarika kwa viwanja vya ndege ndio chachu ya maendeleo kwa sekta nyengine za kiuchumi kama vile utalii na biashara.

Ndugu Wananchi,

Kwa kipindi cha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, huduma za viwanja vya ndege zimeimarika hapa Zanzibar na kuongezeka kwa Makampuni mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa yanayotoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo nje na ndani ya Tanzania.

Hizi zote ni juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo na Muundo wa Umoja wa Kitaifa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar pamoja na kuimarisha uchumi wa Visiwa vya Zanzibar.

Ndugu Wananchi,

Mafanikio yote haya yanatokana na uongozi makini, uadilifu mkubwa, ujasiri wa hali ya juu, ubunifu, mashirikiano na usimamizi mzuri tulionao katika kutekeleza majukumu yetu. Aidha, amani iliyopo Zanzibar pamoja na mshikamano wa Kitaifa uliojengeka miongoni mwa Wazanzibari, umesaidia sana kupatikana kwa mafanikio hayo. Kwani bila ya amani na utulivu hakuna maendeleo. Nawaomba wananchi wote nchini wawe wadau wa kuendeleza amani na utulivu wa nchi yetu.

Ndugu Wananchi,

Sasa napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa kusimamia na kutekeleza majukumu iliyopewa kwa vitendo na kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, naipongeza kwa dhati Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Zanzibar kwa kuimarisha huduma zinazositahiki katika viwanja vya ndege, nawaomba waendelee na moyo huo huo wa kusimamia majukumu yao vizuri kwa lengo la kuwahudumia wananchi Watanzania na nchi nyengine kwa ujumla.

Napenda pia kuupongeza uongozi mpya wa uwanja wa ndege kwa kuboresha mazingira ya uwanja na kuutaka uongozi huo kuzidisha juhudi na ubunifu ili uwanja wetu uwe miongoni mwa viwanja vya ndege vyenye usalama wa hali ya juu wa abiria na usafi wa hali ya juu. Ninayo mifano hai ya viwanja vyengine nje ya nchi ambapo utawakuta wafanyakazi wa usafi wanafanya kazi muda wote wa kazi. Kila saa ufyagio mkononi, wafanyakazi wetu lazima waige mfano huu.

Kwa kipekee kabisa, napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Ndugu Said Ndumbogani pamoja na Meneja wake kwa kuugeuza uwanja huu na kuwa katika hali iliyo sasa, ambao umejaa haiba na kupendeza. Aidha, nautaka Uongozi wa Mamlaka kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa uwanja wa ndege kwa lengo la kuwa na uwezo wa kuwahudumia abiria kwa muda mfupi – shorter check-in times kama inavyowezekana bila ya kuathiri usalama wao na wa abiria.

Pia napenda kuwapongeza kwa dhati TCRA kwa kusimamia usalama wakati wote katika eneo la viwanja vya ndege, Zanzibar. Nawaomba wazidishe mashirikiano yao kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Zanzibar kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. 
 
Vile vile, nawaomba wajenzi wa jengo jipya la abiria pamoja na njia na maegesho ya kutulia ndege kuhakikisha kuwa mradi huu unakamilika kwa wakati uliopangwa. Pia, nawaomba wasimamizi wa ujenzi wa miradi yote miwili kufanya kazi kwa umakini mkubwa na kuhakikisha tunapata jengo jipya la abiria (Terminal II) la kisasa, njia na maegesho ya ndege (Taxway and Apron) zenye kiwango kinachokubalika.

Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mshirika wetu wa Maendeleo hasa Exim Benki ya China na Benki ya Dunia kwa kutuunga mkono katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar. Nawaomba waendelee kushirikiana nasi katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutupatia, misaada na mikopo yenye masharti nafuu.

Nawaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mjenzi wakati watakapo hitajika kufanya hivyo kwa lengo la kufanikisha kazi hii kwa wakati. Vile vile, nawaomba Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kuweka mipaka ya Viwanja vya Ndege Unguja na Pemba kwa lengo la kuepusha uvamizi wa maeneo ya viwanja vya ndege. Hivyo, ningependa kutoa wito kwa wananchi kuheshimu mipaka ya uwanja wa ndege na kujiepusha na kujenga karibu na uwanja huo, jambo ambalo linaweza kuleta usumbufu wakati Serikali inapotaka kufanya upanuzi wa uwanja huo.

Ndugu Wananchi,

Napenda niwapongeze wale wote walioandaa shughuli hii muhimu na kunialika mimi kujumuika nanyi nikiwa Mgeni Rasmi, shughuli ambayo imetayarishwa vizuri na hivyo kufana sana. Aidha, nawapongeza na kuwashukuru wananchi wote ambao wamekuja kwa wingi katika sherehe hii. Naamini kuwa kwa juhudi hizi, wananchi wana kila sababu ya kutuamini na kujenga imani juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya saba kwa kuwapatia maendeleo ya kweli wananchi wa Zanzibar.

Ndugu Wananchi, mwisho ningependa kuwashukuru, msoma quraan, ambaye amesoma aya zenye mnasaba na shughuli yetu hii. Pia nawapongeza wasoma utenzi kwa umalenga wao na kutupa burudani nzuri.

Ndugu Wananchi,

Kwa kumalizia napenda nichukue fursa hii tena kuwapongeza wananchi wote kwa kuhudhuria kwa wingi katika shughuli hii. Naomba Mwenyezi Mungu atuzidishie upendo na utulivu pamoja na kuipenda nchi yetu.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.      

0 comments:

 
Top