Wananchi wa Majimbo ya Donge, Kitope na Bumbwini yaliyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B” wameombwa kuitumia fursa na bahati waliyoipata ya uwepo wa kiwanda cha Sukari Mahonda ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa nafasi za ajira wakati kitakapoanza rasmi kazi zake za uzalishaji wa sukari.

Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa salamu maalum kwenye Mkutano wa hadhara wa Wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Mkaratini ndani ya Jimbo lake la Kitope.

Balozi Seif alisema tabia ya baadhi ya watu kujaribu kufanya hujuma kwa kuchoma moto mashamba yaliyooteshwa miwa ya kiwanda hicho inaweza kuwafukuzisha wawekezaji ambao tayari wameshaonyesha nia ya kutaka kuwekeza vitega uchumi vyao hapa Nchini.

Alieleza kwamba wananchi wa Majimbo hayo wanapaswa kuwa makini pamoja na kukemea vitendo hivyo viovu ambavyo endapo vitaachiliwa kuendelea kufanyika katika maeneo hayo vitachangia kurejesha nyuma juhudi za Serikali kuu za kukaribisha wawekezaji wanaopewa nafasi ya kuwekeza ili kusaidia uchumi wa taifa pamoja na ustawi wa jamii.

“ Vitendo hivyo vinavyofanywa na baadhi ya wenzetu tunapaswa kuelewa kwamba hatuwatendei haki wawekezaji wetu waliojitolea kuweka vitega uchumi vyao hapa Nchini “. Alifafanua Balozi Seif.

Inasikitisha kuona kuwa zaidi ya ekari kumi na nane zilizooteshwa miwa kwa ajili ya usagaji wa sukari wakati utakapoanza uzalishaji tunaarifiwa kwamba zimeteketea kwa moto unaosadikiwa kuwa ni hujuma za makusudi “. Alionyesha Masikitiko yake Balozi Seif.

Aliwashauri wananchi hao kuwa walinzi wa miradi ya uwekezaji ambayo mingi kati yao huwanufaisha wananchi walioziunguukwa na miradi hiyo.

Akizungumzia suala la siasa Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mbunge wa Kitope aliwatahadharisha wana CCM na wanachi wote Nchini kutokubali kudanganywa na baadhi ya wanasiasa wenye sera zisizotekelezeka.

Alisema wanachokihitaji wananchi walio wengi nchini ni sera pamoja na kile wanachokihitaji kitekelezwe na Viongozi waliowachagua katika maeneo yao na si vyenginevyo.

Alifahamisha kwamba baadhi ya wanasiasa hivi sasa wamekuwa kero mitaani kwa tabia yao ya kuendeleza matusi na lawama kiasi kwamba zinakwenda kinyume na mfumo wa vyama vingi vya siasa lakini hata na maadili ya dini.

Aliwataka wananchi kuendelea kuiamini Serikali yao yenye lengo la kuwaletea maendeleo kwa kujenga miundo mbinu itayotoa fursa ya kutanuka kwa huduma za Kiuchumi samba mba na kupunguza umaskini.

“ Tunapaswa tuangalie kwa makini tokea mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 hadi leo Bara bara ngapi zilizojengwa katika maeneo yetu. Sasa lazima tuelewe kwamba Zanzibar ni ya Wazanzibari wenyewe na wao ndio watakaohusika katika kuijenga “. Alisisitiza Balozi Seif.

Aidha Balozi Seif alieleza kwamba lengo la Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha Muungao kwa faida ya watu wake wote.

Alifahamisha kwamba cheche ya ubaguzi inayoendelezwa na baadhi ya watu kwa kutaka kuvunja muungano haiwatendei haki Wazanzibari walio wengi wanaoishi upande wa Bara wa Muungano.

Alisema choko choko hizo zinaendelea kuchochewa wakati tayari wazanzibari hao wameshawekeza miradi kadhaa ya kiuchumi inayoweza kusambaratika kama fitina hiyo ikiachiliwa kuchomoza zaidi.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi alisisitiza na kuweka wazi kwamba msimamo wa Chama cha Mapinduzi uko wazi wa mfumo wa Serikali mbili ambazo ndio muhimili wa kuendelea kuwepo kwa Muungano uliopo hivi sasa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
 

0 comments:

 
Top