Uwanja wa Michezo wa Amani Mjini Zanzibar unatarajiwa kukidhi mahitaji halisi ya maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kutimia miaka Hamsini sawa na Robo karne ifikapo Januani mwaka 2014.

Mahitaji hayo yanafuatia matengenezo makubwa yanayofanywa katika uwanja huo chini ya kampuni ya ujenzi ya Ekika ambayo yanaambatana na uwanja huo kuekewa nyasi bandia zitakazokidhi kiu ya watumiaji wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kuukagua uwanja huo ukiwa katika marekebisho ya mwisho kabla ya kuanza kuwekwa kwa nyasi bandia.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ekika Bwana Ben Mush alimueleza Balozi Seif kwamba wafanyakazi wa Kampuni hiyo walianza kuondoa nyasi asili mwezi Septemba mwaka huu na kuanza kuweka kototo kwa hatua ya kwanza.

Bwana Mush alisema hatua ya pili ilijumuisha uwekaji wa muinuko utakaokidhi umwagaji wa maji kwenye uwanja huo hasa wakati inaponyesha mvua kubwa ambapo kiwango kilichowekwa hakitaruhusu maji kukaa uwanjani si kwa zaidi ya dakika tano.

Alifahamisha kwamba mitaro iliyopo pembezoni mwa uwanja huo hivi sasa iko katika kiwango kinachokubalika.

Balozi Seif pia aliangalia marobota ya nyasi Bandia ambayo tayari yameshawasili Uwanjani hapo zikiwa na ubora wa utafauti kidogo ikilinganishwa na zile zilizowekwa katika uwanja wa michezo wa Gombani Kisiwani Pemba.

Baadaye alikagua maendeleo ya matengenezo ya Hoteli ya Uwanja wa amani na kuuomba uongozi wa Hoteli hiyo kuhakikisha kwamba matengenezo hayo yanakwisha kwa wakati ili hoteli hiyo iweze kutoa huduma samba mba na uwanja huo.

Akizungumza na Uongozi wa Uwanja huo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, pamoja na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar { BTMZ } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza uongozi wa Taasisi hizo kwa mipango mizuri waliyoiandaa ya kufanikisha kazi hiyo.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi na kutoa msaada katika kuona shughuli zote za maandalizi ya uwanja huo pamoja na maandalizi ya mashindano ya Mapinduzi Cup zinafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefikia uwamuzi wa kutaka kuzialika timu za Kimataifa kushiriki katika mashindano yetu ya Kombe la Mapinduzi kutimia Nusu Karne. Sasa lazima maandalizi yetu yawe katika kiwango cha kimataifa “. Alisisitiza Balozi Seif.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni , Utalii na Michezo Dr. Saleh Mwinyikai alisema wakati kazi ya matengenezo ya mwisho ya uwanja huo zikitarajiwa kukamilika wakati wowote kuanzia sasa kitachosubiriwa ni kuwasili kwa gundi la kumaliza kwa kazi ya uwekaji wa nyasi bandia.

Dr. Mwinyikai alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba changamoto liliopo hivi sasa ni kuchelewa kwa meli yenye kontena la gundi hilo.

Hata hivyo Dr. Mwinyikai alieleza kuwa uwekaji wa nyasi hizo unatarajiwa kuchukuwa wiki mbili wakati kontena la gundi hilo kwa mujibu wa Kepteni wa meli inayohusika na m zigo huo inatarajiwa kuwasili nchini Disemba 5 Mwaka huu.

“ Bado tuna matumaini ya kuwahi kwa kukamilisha harakati zetu za matengenezo ya uwanja wetu endapo meli hiyo itafika nchini Mwezi Disemba. Wataalamu wetu wa uwekaji wa nyasi bandia wameeleza kuwa wiki mbili zinatosha kukamilisha kazi hiyo “ Alifafanua Dr. Mwinyikai.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar { BTMZ } Sharifa Khamis { Sherry } alisema zawadi, vikombe pamoja na nishani zitakazotumika katika mashindano ya kombe la Mapinduzi tayari zimesha tayarishwa.

Alisema mashindao hayo yanayotarajiwa kuwa ya kimataifa kwa kushirikisha pia timu za mataifa ya nje yatajumuisha timu karibu 13 zitakazogaiwa kwenye makundi matatu.

“ Tunatarajia mashindano yetu kuwa na timu 13 zitakazogaiwa makundi matatu ambapo mawili yatakuwa Kisiwani unguja na Moja litakuwa Kisiwani pemba ambapo fainali ya mashindano hayo itachezwa Tarehe 13 Januari mwaka 2014 kwenye uwanja wa amani “. Alifafanua Sharifa Khamis.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar { BTMZ } aliupongeza Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kwa ushirikiano uliotoa na hatimae kufikia muelekeo wa hatua ya mafanikio.

Matengenezo ya Uwanja wa Michezo wa Amani Mjini Zanzibar utakaogharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania Milioni Mia Tano { 500.000,000/- } unatarajiwa kukamilika kwake Tarehe 15 Disemba mwaka huu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top