Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesitisha uwepo wa mpaka wa maeneo ya Kilimo baina ya Vijiji viwili jirani vya Muwanda na Pale vinavyopakana Wilaya mbili za Kaskazini B na A ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hatua hiyo ya Serikali imekuja kufuatia kuwepo kwa cheche za shari na dalili za kuibuka kwa vurugu kati ya Wananchi wa Vijiji hivyo jirani ambayo inaonekana kuanza kuchochewa na baadhi ya watu katika misingi na muelekeo wa Kisiasa zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa agizo la kusitishwa kwa mpaka huo uliokiuka Daraja la Kipange wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Muwanda baada ya kupokea malalamiko yao ambayo yalionekana kutokidhi haja katika ngazi ya Shehia, Wilaya hadi Mkoa.

Balozi Seif alisema Wananchi hao wataendelea kutumia mkapa wa asili uliopo ambao ni Mto kwa lengo la kurejesha hali ya utulivu miongoni mwa wananchi wa pande hizo ili wapate fursa za kuendelea na harakati zao za kila siku za kilimo.

Hata hivyo Balozi Seif aliwatanabahisha Wananchi hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mpango wake wa kukabiliana na migogoro ya Ardhi isiyokwisha katika maeneo tofauti Nchini imeshaamua kutengeneza mipaka mipya inayoeleweka katika Wilaya zote za Zanzibar ili kujaribu kudhibiti hali hiyo.

“ Tumefikia wakati kutengeneza mipaka mipya na kuachana na ile tuliyoizoea kama mito ambayo tumekuwa tukishuhudia migogoro isiyokwisha. Upo Mfano hai wa Ziwa Nyasa linaloigawa Tanzania na Malawi ambapo sheria za Kimataifa zinaeleza kuwa mpaka unakuwa kati kati ya ziwa. Sasa upande wa wenzetu wanalalamika kwamba Ziwa Nyasa ni mali yao”. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali wakati wote isingependa kuona Wananchi wake wanaendelea kupata matatizo yanayoweza kuepukwa kwa njia ya kistaarabu na mazungumzo badala ya vurugu.

Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi hao wa Kijiji cha Muanda waendelee kuiamini Serikali yao kwa vile ipo madarakani maalum kwa kuwatumikia wananchi wake.

“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo hivi sasa tumeshaamua kuiendesha katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa haitothubutu kuwafanyia ubabe Wananchi wake. Sisi Viongozi wa juu wa Serikali tungelipenda kuona Wananchi wetu wanaendelea kulima vizuri. Wanaishi vizuri bila ya fujo wala bughdha “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi hao wa Kijiji cha Muanda kwa uvumilivu wao mkubwa waliouchukuwa licha ya ushawishi mkubwa uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wana siasa wa kutaka kufarakanisha Wakazi wa Vijiji hivyo jirani kinasabu.

“ Kuanzia leo natoa agizo la kusitisha suala la kuwepo mpaka kati ya Vijiji vya Muanda na Pale “. Alimalizia Mazungumzo yake Balozi Seif kwa msisitizo huo ulioonekana kuungwa mkono na kundi kubwa la Wananchi hao wa Kijiji cha Muanda.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaahidi Wananachi wa Kijiji hicho cha Muanda na Kile cha Jirani cha Pale kwamba atafanya ziara maalum katika kipindi kifupi kijacho kuangalia eneo hilo la mpaka ili kujionea mazingira yaliyopo na kupata fursa ya kufungua ukurasa mpya wa kurejesha mashirikiano yaliyopo ya zamani ya pande hizo mbili.

Mapema Wanakijiji hao wa Muanda walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba chanzo cha tatizo hilo kinatokana na Uongozi wa zamani uliopita wa Shehia na CCM Kijijini hapo kuhodhi eneo kubwa la ardhi lililonyima haki na fursa wananchi wa maeneo hayo mawili kuendeleza shughuli za Kilimo.

Bwana Abdulla Ambari Mustapha akifafanua kwa ufasaha hitilafu ya mzozo huo wa mpaka alimueleza Balozi Seif kuwa uzoefu wa zamani unaonyesha wazi kwamba wananchi na wakulima wa Kijiji cha Pale walikuwa wakilima katika bonde la Muanda kwa mashirikiano mazuri.

Alifahamisha kwamba ushawishi uliokuwa ukifanywa na uongozi wa zamani wa shehia na Tawi Kijijini Muanda ulipelekea kuibuka kwa baadhi ya watu wa Kijiji cha Pale kuamua kuvamia mashamba hayo na kuweka mipaka mipya bila ya kufuatwa ule uliozoeleka wa zamani ambao ni mto.

“ Tunapaswa kuwa wazi katika hili. Ukweli ni kwamba tatizo hilo limesababishwa na Sheha aliyepita bila ya kumtaja jina ambae aliamua kujilimbikizia mashamba kwa kushirikiana na familia yake ambapo pia alitoa upendelea wa kutumiwa mashamba hayo kwa baadhi ya wakulima wa Kijiji cha Pale “. Bwana Ambari alionyesha kukerwa na kitendo cha Sheha huyo.

Kijiji cha Muanda kiko katika Wilaya ya Kaskazini “B” kikipakana na kile cha Pale kilichoko Wilaya ya Kaskazini “ A “ vikijumuisha kuunga Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top