Serikali ya Ras Al – Khaimah na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetiliana saini mkataba utakaotoa fursa kwa Wataalamu na Wahandisi wa Kampuni ya Kimataifa ya utafiti na uchimbaji wa mafuta na Gesi ya Ras Al –Khaimah { Ras Gas } kufanya utafiti wa awali { SCAUT } katika maeneo ya ardhi na Baharini ili kupata uhakika wa uwepo wa rasilmali ya mafuta na Gesi Zanzibar.

Mkataba huo umetiwa saini katika hafla maalum iliyofanyika katika Jumba la Kifahari la Kifalme la Al - Dhait Palace Nchini Ras Al – Khaimah na kushuhudiwa na Mfalme wa Nchi hiyo Sheikh Saud Bin Saqr Al – Qasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiuongoza Ujumbe Mzito wa Mawaziri Saba wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa Upande wa Zanzibar Saini hiyo imetiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Nd. Ali Khalil Mirza wakati ule wa Rais Al – Khaimah imewekwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya utafiti na uchimbaji wa Mafuta na Gesi ya { Ras Gas } Bwana Kamal Ahaya.

Mawaziri walioshuhudia kitendo hicho ambacho kinaweka kihistoria mpya kwa Zanzibar ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed, Waziri wa Feha Mh. Omar Yussuf Mzee, Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban na Waziri wa Afya Mh. Juma Duni Haji.

Wengine walioshuhudia ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Kazi na Utumishi wa Umma Mh. Haroun Ali Suleiman, Mwanasheria Mkuu wa SMZ Mh. Othman Masoud Othman, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Nd. Khamis Mussa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi, Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Utumishi wa Umma Bibi Asha Abdula, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Abdulla Mzee Abdulla pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar Nd. Salum Khamis.

Kampuni hiyo ya Utafiti na Uchimbaji wa Gesi ya Ras Gas iliomba kufanya kazi hiyo kwa karibu miezi sita iliyopita jambo ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ililazimika kuwa na hadhari na suala hilo kabla YA kutoa uwamuzi muwafaka na sahihi.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iliwahi kuipa Kampuni ya Antrim kufanya utafiti Zanzibar na Tanzania kwa ujumla lakini Kampuni hiyo ililazimika kukatisha kazi hiyo baada ya mwaka 2009 kuibuka hoja ya Zanzibar kutaka kusimamia yenyewe Rasilmali hiyo ya Mafuta na Gesi.

Tafiti za awali zinaeleza kwamba zipo ishara na dalili zinazoonyesha uwepo wa rasilmali ya mafuta na Gesi katika baadhi ya maeneo ya ardhini na Baharini ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

Utafiti uliowahi kufanywa katika Kisiwa cha Pemba mnamo Mwaka 1982 umeelezwa kuwepo kwa ishara hiyo inayotoa matumaini ya Zanzibar kuingia katika harakati za uchumi mwengine badala ya ule iliyouzoea wa Karabuu ukisaidiwa na Sekta ya Utalii.

Kampuni za Kimataifa za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi za Ras Gas na ile ya Shell ziliwahi kujitokeza kuomba fursa ya kufanya utafiti wa rasilmali hiyo kipindi kilichopita.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top